Caf Yampaisha Kagere Tuzo ya Mchezaji Bora wa Afrika
0
November 28, 2019
ZIKIWA zimepita siku chache tangu Shirikisho la Soka Afrika (CAF), kumtangaza mshambuliaji wa Simba, Meddie Kagere kuwa miongoni mwa wachezaji wanaowania Tuzo ya Mchezaji Bora wa Afrika kwa wale wanaocheza ligi ya ndani, sasa mchezaji huyo si wa mchezomchezo baada ya wakala wake kusema anayemhitaji sasa atoe bilioni 1.5.
Kagere amepata nafasi hiyo kutokana na kiwango cha juu alichoonyesha msimu uliopita akiwa na kikosi cha Simba katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuiongoza timu hiyo kufika hatua ya robo fainali ya michuano hiyo lakini pia yeye mwenyewe akishika nafasi ya pili kwa kuzifumania nyavu baada ya kufunga mabao sita.
Wakala wa Kagere, Patrick Gakumba ameliambia Championi Jumatano kuwa kutokana na hali hiyo thamani ya Kagere sasa imeongezeka mara mbili zaidi ya ile aliyokuwa nayo hapo awali. Alisema hapo awali thamani ya
Kagere ilikuwa ni kuanzia dola 300,000 (zaidi ya Sh milioni 685) lakini kwa sasa timu yoyote ambayo itamhitaji itabidi itoe dola 500,000 (zaidi Sh bilioni 1.143).
“Kusema kweli baada ya kusikia kuwa Kagere amechaguliwa kuwania Tuzo ya Mchezaji Bora Afrika, nilifurahi sana kwani sasa thamani yake imeongezeka ukilinganisha na ilivyokuwa hapo awali, hakika namshukuru sana Mungu.
“Kwa sasa tunaendelea kumuomba Mungu ili aweze kutusaidia Kagere aweze kuibuka mchezaji bora kwa sababu vigezo anavyo, aliibuka mfungaji bora namba mbili katika michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika. “Ikitokea akaikosa nafasi hiyo basi hata hapa alipofikia ni sehemu nzuri kwani tayari thamani yake imeongezeka siyo tena wa dola 300,000 sasa ni dola 500,000 na kuendelea.”
Tags