Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA , kimewataka Wagombea wa chama hicho ambao wameenguliwa kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa kwa madai kuwa wamekosea kujaza fomu zao kukata rufaa.
Akiongea na Waandishi wa habari Mkurugenzi wa Itifaki na Mambo ya Nje wa CHADEMA, John Mrema mbali na hilo ameeleza kuwa wataitisha vikao vya dharura kujadili hali hiyo ambayo wamedai kuwa imejitokeza katika maeneo mengi nchini.
“Hadi sasa tunazungumza hapa, wagombea wote wa Chadema Mkoa wa Simiyu, Wilaya ya Ngala (Kagera), Jimbo la Ubungo (Dar es Salaam), Jimbo la Mbeya Mjini na Busokelo wote na maeneo mengine wameondolewa. Wanaenguliwa na wasimamizi hawatoi sababu licha ya kanuni kuwataka kufanya hivyo.
“Tunajiuliza hivi mitaa 192 yote yaani hajakosekana hata mgombea mmoja hata wale waliokuwa wenyeviti wakaamua kugombea tena, wameshindwa kujaza fomu?,” amedai Mrema.
Amesema kutokana na hali hiyo, Chadema kimeitisha vikao hivyo vitakavyoanza kesho kujadili mwenendo huo na kutoa msimamo wa chama na hatua watakazozichukua kutokana na sintofahamu hiyo.