Freeman Mbowe Aanza Kujitetea Mahakamani........"Sikuwepo Kwenye Maandamano. ni Hisia tu"


Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa hakuwepo kwenye maandamano ya wafuasi wa chama hicho yanayodaiwa kusababisha kifo cha Mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji (N.I.T) Akwilina Akwelini.

Mbowe ameyaeleza hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba wakati akitoa utetezi wake katika kesi inayomkabili na viongozi wenzie 8 wa CHADEMA.

Mbowe alitoa ushahidi wake akingozwa na wakili wa utetezi, Peter Kibatala ambapo  amedai hakuwepo eneo la maandamano na kama ilitolewa amri ya Polisi yeye hawezi kukataa kutawanyika kwa sababu hakuwepo, hivyo ni hisia za Polisi tu zimeeleza kwamba alikuwepo.

Amedai kuwa baada ya kumaliza mkutano wa kufunga kampeni katika Uwanja wa Buibui Mwanyamala aliondoka uwanjani hapo akiongozwa na Askari Polisi kuelekea Makao Makuu ya CHADEMA Kinondoni.

Amedai siku hiyo wahudhuriaji wa CHADEMA wakiwa njiani walikutana na wahudhuriaji wa CCM katika makutano ya barabara ya Morocco na Mwananyamala wakiwa na mgombea wao wakisindikizwa na ngoma aina ya Mdundiko.

Mbowe amedai kuwa wanachama hao wa CHADEMA walikuwa wakiongozwa na Polisi kuelekea barabara ya Morocco ambapo yeye hakujua kilichoendelea nyuma kwani aliendelea na safari yake ya kuelekea Makao Makuu ya CHADEMA.

Akizungumzia kufikishwa kwake Mahakamani Mbowe amedai kuwa kwa mara ya kwanza alipokea wito wa kuitwa Polisi kupitia mkutano wa waandishi wa habari ulioitishwa na Kamanda wa Polisi Kanda maalumu Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa.

Amedai kuwa Kamanda huyo wa Polisi alitoa wito kwa viongozi wa CHADEMA kuripoti polisi kuhusiana tukio hilo la maandamano.

Pia amedai kuwa alipata taarifa kuhusu kifo cha Akwilina Akwiline aliyepigwa risasi katika maandamano hayo kupitia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari na kwamba Polisi inawashilikia askari kuhusu tukio hilo.

Mbowe amedai kuwa hajawahi kula njama na washtakiwa wenzake bali waliitwa kwa nyakati tofauti kwenda Polisi.

Mbali na Mbowe washitakiwa wengine katika kesi hiyo, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Salum Mwalimu, Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya.

Baada ya kutoa ushahidi huo, upande wa utetezi ukaomba shauri hilo liahirishwe hadi siku nyingine kwa sababu mshitakiwa wa Tisa, Ester Bulaya anaumwa.

Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi Novemba 8, 2019.

Wengine ni Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa, Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Vincent Mashinji.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad