Mbunge wa jimbo la Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema,amesema ameshangazwa na jeshi la polisi kwenda kufanya upekuzi nyumbani kwa mchekeshaji na mshindi wa shindano la Big Brother 2014, Idris Sultan ina maana aliiba kiti cha Rais.
Lema aliandika ujumbe huo kupitia ukurasa wake wa Twitter kuwa baada ya ule utani wa kawaida alioufanya siku ya kuzaliwa Rais John Magufuli alijisalimisha polisi akiwa chini ya ulinzi.
Alisema alipelekwa nyumbani kwake kwa ajili ya upekuzi.
“Sasa najiuliza polisi mlienda kusachi nini au mlifikiri Idris ameiba kiti cha Rais? Uoga unaondoa maarifa na busara,” alisema Lema.
Baada ya ule utani wa kawaida sana aliofanya siku ya kuzaliwa Rais,Idris Sultan alijisalimisha Polisi akiwa chini ya ulinzi alipelekwa nyumbani kwake kwa upekuzi.Sasa najiuliza Polisi mlienda kusachi nini au mlifikiri Idris ameiba kiti cha Rais ?Uoga unaondoa maarifa na busara— Godbless E.J. Lema (@godbless_lema) November 1, 2019
Oktoba 30, 2019 mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alimtaka Idris kuripoti polisi baada ya kuweka picha yenye sura yake huku akiwa ameketi katika kiti chenye nembo ya Taifa.
Pia, Idris aliweka picha nyingine inayoonyesha sura ya Rais Magufuli akiwa amesimama huku amevaa suruali yenye mikanda inayoshikizwa mabegani.
Hata hivyo, dakika chache baada ya Makonda kumtaka msanii huyo kuripoti polisi, waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla aliahidi kumuwekea dhamana iwapo angekamatwa.
Jana alihojiwa Idris na kisha polisi kwenda nyumbani kwake kufanya ukaguzi.