Msemaji wa Serikali ya Tanzania, Dkt. Hassan Abbas kupitia ukurasa wake wa Mtandao wa Twitter amevionya Vyombo vya Habari Nchini alivyodai vinatumiwa na Mataifa ya Nje kusambaza habari za Uongo dhidi ya Tanzania
Amesema, "Katika siku za karibuni kumeibuka tena tabia ya baadhi ya Vyombo vya Habari hapa nchini kushabikia, kutumika na kuwa Mawakala wa kusambaza habari za uongo, uzushi na propaganda dhidi ya nchi yetu kutoka Mashirika ya Kimataifa au Wawakilishi wa Mataifa ya Nje."
Ameongeza, "Bahati mbaya katika habari hizo Misingi ya Taaluma ya Habari husiginwa hasa Kanuni ya kujiridhisha na ukweli wa tuhuma husika. Serikali imeelekeza vya kutosha, imeonya vya kutosha na imesamehe vya kutosha, sasa tutachukua hatua kali za Kisheria."
Amesisitiza, "Vyombo vya Habari vya Ndani na Nje ya nchi vilivyosajiliwa, kupewa ruhusa ya kutekeleza majukumu yao hapa Nchini vinakumbushwa tena kuwa Uandishi wa Habari ni Taaluma. Ina Haki zake, Wajibu wake, Misingi yake na zaidi Sheria zake.”