Jaji Mkuu Kenya Atishia Kususia Majukumu yake
0
November 05, 2019
Jaji Mkuu wa Kenya David Maraga ametishia kususia majukumu yake ya kikazi kufuatia kukatwa kwa bajeti ya mahakama.
Hivi karibuni serikali ya Kenya ilipunguza zaidi ya dola milioni 30 kutoka kenye bajeti ya mwaka ya sekta ya mahakama , hatua ambayo Bwana Maraga anadai inalenga kudhibiti Mahakama.
Maraga ambaye alionekana mwenye hasira katika hotuba yake kwa taifa kwa njia ya televisheni, amefichua madai ya kile alichosema ni njama za serikali za kumuondoa madarakani kabla ya tarehe 31 Disemba.
"Baadhi ya mawaziri wanasema nitakwenda kabla ya mwisho wa mwaka huu , kumbe hii Kenya ina wenyewe ?" alisema Maraga.
Amedai pia kwamba kupunguzwa kwa bajeti ya mahakama lilikuwa ni jaribio la makusudi la kukwamisha shughuli zake.
Bwana Maraga amesema kuwa baadhi ya vikao vya mahakama kote nchini vimeahirishwa pamoja na pesa zilizopangwa kwa ajili ya kuharakisha shughuli za mahakama zimekatwa.
Jaji huyo mkuu nchini Kenya amedai kuwa ofisi yake haiwezi hata kupata bajeti zilizoidhinishwa, na kwamba mahakama inahangaika kupata huduma muhimu kama vile Wi-Fi na mafuta ya gari.
Anadai maafisa wa kitaifa ambao hakuwataja majina walidai kuwakanganya majaji ambao walishindwa kutoa uamuzi wa kesi zilizoingiliwa, hususan kesi maarufu za ufisadi zinazowahusisha maafisa wa umma wa ngazi ya juu.
Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, bajeti ya mwaka ya Kenya imeongezeka, lakini katika kipindi hicho bajeti ya mahakama imepunguzwa.
Katika mwaka huu wa fedha taifa hilo lilitangaza bajeti ya dola bilioni 30, ni dola milioni 170 au 0.6% ya bajeti zilizotengwa kwa ajili ya idara ya mahakama kabla ya kupunguzwa hadi dola milioni 140 mnamo mwezi Septemba.
Jaji Mkuu alisema kuwa kwa kawaida mahakama hutengewa asilimia 2 ya bajeti ya kila mwaka ya taifa kote duniani, ikimaanisha kuwa walipaswa kupokea takriban dola milioni 600.
Lakini mwaka huu serikali ilitangaza kuwa haina pesa na kukata bajeti kote katika idara na mashirika mbali mbali nchini humo.
Huku Jaji Mkuu akikiri kuwa Kenya inapitia vipindi vigumu kiuchumi, asisitiza kuwa pesa zilizopo hazijagawanywa kwa usawa.
Mahakama nchini Kenya imekuwa na msuguano na serikali ya Kenya, tangu Mahakama kuu ilipobatilisha ushindi wa rais Uhuru Kenyatta katika uchaguzi wa mwaka 2017.
Alipochaguliwa kwa mara ya pili, rais Kenyatta aliwatika majaji 'wahalifu' na akaahidi ' kukabiliana ' na Mahakama
Tags