Kila mmoja wetu anatamani au kupenda kuwa katika mahusiano yenye furaha na amani. Kila mmoja anapenda kuwa na mpenzi mwenye mapenzi ya kweli na pasiwe na chembe za kusalitiana.
Tunaishi katika ulimwengu wenye changamoto nyingi na kiwango cha uaminifu kinazidi kushuka kila kukicha. Katika hali kama hiyo watu wengi wamejikuta wapo njia panda wasijue washike wapi au waachie wapi kwenye suala zima kuwa kwenye mahusiano. Leo ningependa kushirikiana nanyi katika namna nzuri ya kumpata yule mwenye kukidhi matakwa ya nafsi yako hata katika nyakati hizii ngumu na za tabu kama ifuatavyo:-
Badilisha mtazamo wako na mfumo wa maisha yako
Kwa ukawaida watu tunaokutana na kushirikiana nao kwenye maisha yetu ni watu waliovutwa na namna sisi tulivyo ambapo kupitia watu hao ndio unapata taswira kuwa wewe ni mtu wa aina gani.
Tunapata wapenzi wa hovyo hovyo kwa kuwa sisi wenyewe ni wa hovyo hovyo
Tunapata wapenzi wasio waaminifu kwa kuwa tunajiweka katika mazingira ya kutoaminika
Tunapata wapenzi wa kututumia na kutuacha kwa kuwa tumejiweka katika mtazamo wa kutumiwa na kuachwa
Jinsi tunavyojiweka ndivyo tunavyowavutia watu wa kaliba yetu. Kabla ya kuweka masharti yako ya mpenzi umtakaye kwanza unatakiwa ujiangalie wewe mwenyewe kuwa unaendana na sifa hizo? Mfumo wako wa maisha unawavutia watu wa aina hiyo?
Utakuja kugundua kuwa hata wewe mwenyewe haufanani na hilo unalolitaka, sasa utapataje kitu usichofanana nacho? Ndege wafananao huruka pamoja. Unatakiwa kwanza ubadilike ili watu wazuri waje kwenye maisha yako!!!
Rahisisha mahitaji yako
Katika ulimwengu wa nyama na roho hakuna mkamilifu kati yetu kwa hiyo ni vigumu kumpata mtu mwenye sifa zote unazozitaka wewe kwa kuwa hukushiriki hata chembe kwenye uumbaji huo. Hata wewe mwenyewe una mapungufu yako tena pengine ni makubwa sana isipokuwa waungwana kwa kuwa wanajua kuwa hakuna mkamilifu wanaamua kukuvumilia.
Weka mahitaji yako machache na yale ya msingi. Watu wanadumu kwenye mahusiano si kwa kuwa ni wakamilifu bali kwa uvumilivu na kusameheana. Toka katika ulimwengu wa fikra pambana na hali halisi. Watu wengi wamejijengea taswira nzuri za mahusiano katika ulimwengu wa kufikirika. Taswira nzuri walizojijengea na kuishi nazo ni ngumu kuziweka katika hali ya kawaida kwa kuwa nafsi zao zina matarajio makubwa kupita ukweli ambao upo mezani.
Matokeo ya watu hao ni kubadilisha wenzi kila mara kwani wanapambana kuuridhisha ulimwengu wa nafsi. Ndio hao unakuja kuona anakwambia nataka mwanamume awe mrefu kidogo, mweusi kidogo, awe na vibonyeo kwenye mashavu na awe na kifua kilichojengwa kimazoezi wenyewe wanasemaga six pack.
Wanaume nao utawasikia nataka mwanamke mwenye urefu wa wastani, awe na umbo namba nane, maziwa yaliyojaa vyema kifuani na awe na neema za Allah. Kwa kawaida hayo ni maelezo yanayotoa taswira ya kupendeza lakini katika ulimwengu halisi ni ngumu kukidhi matakwa hisia hizo.
Kuwa na subira
Wahenga walinena kuwa subira huvuta kheri. Wakati mwingine mambo mazuri yanachelewa kutufikia kwani siku zote mambo hayawezi kuwa kwa jinsi tunavyotaka sisi. Kwahiyo unapaswa kuwa na subira. Wengi wamejikuta wameangukia kwenye maumivu makali ya moyo baada ya kukosa subira.
Wakati mwengine subira kidogo tu inaweza ikatuokoa na majanga makubwa sana. Siku hizi imekuwa sio jambo la ajabu kuona amekutana na mwanamke leo na leo wakaenda kufanya ngono na kesho yake wanatangaza ndoa. Sasa sijui itakuwa ndo ya aina gani kama sio kituko?
Nawasilisha.