JPM: CAG Usijifanye na Wewe ni Mhimili, Usibishane na Bunge
0
November 04, 2019
Rais John Magufuli amemuapisha Charles Kichere kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) akichukua nafasi ya Prof. Mussa Assad aliyemaliza muda wake leo Novemba 4, 2019. CAG Kichere alikuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe na kabla ya hapo alikuwa Kamishna Mkuu wa TRA.
Magufuli amewaapisha pia viongozi mbalimbali kama Katibu tawala mkoa wa Njombe, Balozi wa Tanzania Nchini Kuwait, Kamishna wa kazi katika ofisi ya waziri mkuu na majaji 12 wa mahakama kuu.
Akizungumza mara baada ya kuwaapisha viongozi hao Rais Magufuli amesema;
“CAG mpya usiende huko ukajifanya na wewe ni mhimili, mihimili ni mitatau tu; Bunge, Mahakama na Serikali, nimesikiliza kiapo chako ni Mkaguzi wa Hesabu za Serikali, kwa hiyo mwenye Serikali yupo. Unapopewa maagizo na mihimili kama Bunge, tekeleza usibishane nao, wewe ni mtumishi.
“CAG kuna baadhi ya watendaji wako utawakuta huko, wanapotumwa kwenda kukagua kwenye balozi wanalipwa pesa hapa, wakifika kwenye balozi napo wanapewa pesa, sitaki kuwataja majina yao, wewe nenda kachambue mwenyewe. Ofisi ya CAG siyo safi kama mnavyodhani, kaipangue hiyo ofisi na uisafisahe.
“Huwa hatukosei kuteuwa, CAG mpya ulipata division 1 form IV, division 1 form VI, hii inaonesha wewe sio kilaza ni panga. Una digrii ya sheria, ukachukua na digrii ya accounts ukatoka na Hons, ukachukua masters, umefanya kazi mahali pengi, kwa hiyo tunakuamini.
“CAG Kichere una heshima, tulipokuondoa ukamishna wa TRA tukakupeleka u-RAS hukusema chochote, umeenda ukapiga kazi, una heshima. Wengine ukiwateua utadhani nafasi ni zao, unampa u-DC ukimtoa analalamika, kwa nini hukulalamika wakati nakuteua? Nenda kapige kazi.
“Nataka nikueleze kabisa, katiba na sheria zinazungumza na, unaweza kukaa miaka 5 ya mkataba wako, pia unaweza kukaa mwaka 1 ukatoka, taratibu za kukutoa zipo na zinafanywa na Rais, sikutishi. Huwezi kupewa mamlaka ya kuteua ukashindwa kutengua utakuwa hufai kuwa Rais,” amesema Rais Magufuli.
Aidha Spika Job Ndugai amezungumza; “CAG Kichere karibu sana, sisi Bunge tunaanza shughuli zetu kesho za kuangalia mipango ya Taifa ambayo inaweka vipaumbele ambavyo vitaisaidia Serikali kuona ni aina gani ya Bajeti ya Serikali ambayo itakuja 2020/21, wewe CAG ndio jicho letu tunakutegemea,”- Spika Job Ndugai.
Tags