Kocha msaidi wa taifa ya Tanzania 'Taifa Stars', Juma Mgunda ametoa ufafanuzi wa kauli yake aliyoitoa hivi karibuni, ambayo imezua gumzo baada ya kuzungumzia kuchwa kwa golikipa Aishi Manula.
Mgunda amesema kuwa wanaosambaza kauli yake wamechukua neno moja tu badala ya kutafsiri sentensi nzima aliyoizungumza kuhusiana na suala hilo.
"Naomba nitoe msisitizo kwamba taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zilininukuu vibaya na kilichofanyika ni kwamba lilichukuliwa neno moja na sio sentensi nzima. Mimi nilieleza kuwa wachezaji waliochaguliwa kwa kipindi hiki ndiyo wachezaji wanaofaa kwa kuzingatia hali halisi ilivyo kwa sasa.", amesema Mgunda.
Katika kauli yake aliyoitoa juzi, wakati wa mazoezi ya Taifa Stars katika uwanja wa taifa, Mgunda alisema kuwa Manula hakuitwa Stars kwa sababu wao kama makocha hawaendi kupeleka posa na badala yake wanaangalia wachezaji wanaowaona wanastahili katika wakati husika.
Ikumbukwe Taifa Stars inaendelea na maandalizi yake kujiandaa na mchezo wa kuwania kufuzu michuano ya AFCON 2021 nchini Cameroon, ambapo itacheza na Equitorial Guinea, Novemba 15 katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.