Lugola: Laini za Simu Ambazo Hazijasajiliwa Hazitazimwa
0
November 14, 2019
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amesema hakuna Mtanzania yeyote ambaye simu yake itazuiwa kutumika, kwa sababu hajasajili, kwa kigezo cha kutokuwa na Kitambulisho cha Taifa.
Kwa maana hiyo, ikifika Desemba 31 mwaka huu, ambayo ni mwisho wa kusajili laini za simu kama mtu hajapata kitambulisho cha taifa, laini yake ya simu haitazimwa na ataendelea kuitumia.
Aidha, Lugola amemwagiza Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho Vya Taifa (NIDA), kuhakikisha kwamba maofisa wa NIDA wilaya zote, wanapeleka namba za vitambulisho vijijini ; na si kutegemea kuzipata katika simu.
Lugola ametoa kauli hiyo bungeni mjini Dodoma jana Jumatano Novemba 13, 2019 wakati akijibu mwongozo wa mbunge wa Kavuu (CCM) Dk Pudensiana Kikwembe.
Katika mwongozo wake alisema uandikishaji wa vitambulisho vya taifa, umekuwa na changamoto maeneo ya vijijini.
Alisema kuwa tatizo hilo limekuwa kubwa hasa vijijini hususani majimbo ya Kavuu na Mlele, ambako uandikishaji umekuwa ni shida.
“Kama inavyojulikana mwisho ni Desemba mwaka huu, naomba kujua kauli ya serikali nini kinafanyika ili waweze kupata vitambulisho,”alisema Pudenciana.
Akijibu mwongozo huo, Lugola aliwatoa hofu wasiwasi Watanzania kuwa utaratibu wa utambuzi, usajili na utoaji wa vitambulisho kwa wananchi, ambao wana sifa za kupata vitambulisho ni endelevu.
“Zoezi hili halina mwisho wala halina tarehe kwamba ikifika tarehe fulani kuna Mtanzania hajapata kitambulisho, basi huyo Mtanzania hatapata kitambulisho tena, Watanzania wasiwe na wasiwasi, hili ni zoezi endelevu na ndio maana kila mwaka kuna Watanzania ambao wanafikisha miaka 18.” alisema.
Akizungumzia suala la usajili wa laini kwa vidole, Lugola alisema: “Naomba niwatoe wasiwasi Watanzania wote kwamba maelekezo Rais John Magufuli hakuna Mtanzania ambaye simu yake itazuiwa kutumika eti kwa sababu hana kitambulisho cha taifa na hivyo hajasajili laini yake.”
Tags