Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeamuru wabunge wanne wa CHADEMA, Ester Bulaya, Halima Mdee, Peter Msigwa, na John Heche wakamatwe na kufikishwa mahakamani hapo kwa kukiuka masharti ya dhamana.
Amri hiyo imetolewa leo na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba baada ya wabunge hao kutokuwepo mahakamani bila taarifa yoyote. Hata wadhamini wao pia hawakuwepo.
Pia, Hakimu Simba ametoa hati ya wito wa wadhamini wa wabunge hao kujua sababu za kutowapeleka washtakiwa mahakamani.
Kabla ya kutoa amri hizo, Hakimu Simba amesema leo kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa, washtakiwa wengine waliwahi lakini wabunge hao wanne hadi saa 4:05 asubuhi walikuwa hawajafika mahakamani bila sababu za msingi.
Baada ya Hakimu Simba kueleza hayo wakili wa upande wa utetezi, Faraji Mangula aliyewawakilisha mawakili Profesa Abdallah Safari, Peter Kibatala na Jeremiah Mtobesya ameieleza mahakama hiyo kuwa ana taarifa za Bulaya.
Kauli ya Mangula ilipingwa na Hakimu Simba aliyebainisha kuwa anayepaswa kuzungumza kuhusu washtakiwa kutofika mahakamani ni wadhamini si wakili.
Kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 13, ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia na kuhamasisha hisia za chuki.