KABLA sijaanza kukufungulia Ukurasa mpya, bila shaka utakumbuka katika toleo la wiki iliyopita tulihitimisha simulizi safi kabisa kutoka kwa mrembo ambaye anafanya vyema katika soko la muziki wa kizazi kipya, Winifrida Josephat au Dotto kwa jina halisi la kuzaliwa ingawa anajulikana zaidi kwa jina la Recho.
Leo nakuanzishia safari mpya ya kuyajua maisha ya msanii mwingine ndani ya Muziki wa Bongo Fleva ambaye kwa namna Fulani tunaokumbuka kwenye miaka ya 2013/2014, hutabishana na mimi kuwa kipindi hicho kulikuwepo na kijana mmoja aitwaye Malima au ukipenda kumuita kwa jina la ubatizo anajulikana kama Laurent Madole. Jina lake la kisanii ni Marlaw.
Historia yake ya maisha anasema kuwa, yeye ni mzaliwa wa Mkoa wa Arusha, ambapo alizaliwa mwaka 1984, katika Hospitali ya CTU ambayo kwa sasa inajulikana kama TMA ambayo ni Hospitali ya Jeshi, iliyopo Wilaya ya Monduli huko Arusha, akiwa ni mtoto wa tano kuzaliwa katika familia yao yenye watoto sita. Wa kiume watatu na wa kike idadi kama hiyo. Baba yake mzazi ni Mpare na mama yake ni Mgogo wa Dodoma.
Marlaw anasema kuwa ukitaka kujua zaidi yeye anatokea katika familia yenye uwezo gani, basi tambua kuwa ni miongoni mwa vijana waliozaliwa katika familia za kawaida tu.
Huyu hapa Marlaw anatiririka mwenyewe: “Kwa ufupi mimi naweza kusema natokea katika familia ya kawaida tu yaani yenye maisha ya kati kwani baba yangu alikuwa ofisa mstaafu wa jeshi akijulikana kama Meja Madole, lakini mama yangu ambaye kwa sasa ni marehemu, alikuwa ni askari wa Jeshi la Magereza.
“Kwa maana hiyo naweza kusema wazi kuwa mimi ni miongoni mwa Watanzania wengi waliotokea kwenye familia yenye uchumi wa katikati na wa kawaida tu na wala siyo watu wa maisha ya juu wala ya chini sana.
“Lakini kitu ambacho wengi wanatakiwa kujua kwa nini nasema tulikuwa na maisha ya kati ni kwamba katika familia yetu wengi wetu tuliishi kwa muda mrefu na mama yetu baada tu ya kutengana na baba kwenye mwaka 1987, hivyo tukalelewa upande mmoja zaidi wa mama hadi naye alipokuja kufariki kwenye mwaka 1997 mimi nikiwa na umri wa miaka kama 14, hivyo tukalazimika kugawanyika kila mmoja akaenda kulelewa mahali kwingine.
“Mimi nilichukuliwa na mama yangu mdogo kwenda kulelewa Shinyanga na ndipo nilipoendelea kusoma darasa la tano hadi kidato cha nne nilipomalizia.
“Huwezi kuamini tangu alipofariki mama yangu na mimi kwenda kulelewa Shinyanga, sikupata kuonana na baba yangu tena hadi baada ya miaka 20, maana nakumbuka tumekuja kukutana tena mwaka 2007, ingawa namshukuru Mungu pamoja na kutoishi naye kwa kipindi chote kile lakini tulipokuja kukutana maisha yaliendelea vizuri hadi sasa ninaishi naye kwa amani na furaha tele.
“Kwa ufupi historia yangu ya masomo nilianza kusoma Shule ya Msingi Bruka Estate ipo Arusha mwaka 1993, ilikuwa karibu tu na hapo Gerezani tulipokuwa tukiishi, maana mama yangu alikuwa askari pale, hapo nilikuwa na umri wa miaka kama tisa hivi.
“Nakumbuka nililazimika kurudi nyuma darasa moja maana kabla ya mama kufariki tulilazimika kukaa nje ya masomo kwa muda mrefu sana karibia wote tuliokuwa tukisoma nyumbani kwetu.
“Baada ya hapo mama alihamishiwa katika Gereza la Kilimo la Mang’ola lipo Wilaya ya Karatu, hivyo baada ya kufika pale nikaendelea kusoma darasa la pili hadi darasa la tano ambapo ndiyo aliugua na kufariki nikiwa darasa hilo na sisi wadogowadogo watatu tulitawanywa kwenda kwa mama zetu wadogo na baba zetu.
“Wale wakubwa kama kaka yetu yeye tayari alikuwa mwanajeshi, mwingine alikuwa mfanyabiashara na wa tatu ambaye ni dada yangu yeye alikuwa tayari ni msanii.
“Naamini wengi hawajui kuwa fani ya usanii kwetu ipo kitambo tu, maana enzi mama amekufa dada yangu aitwaye Rayah yeye tayari alikuwa ameshaingia kwenye sanaa ya maigizo katika Kundi la Kaole jambo ambalo wengi hawawezi kufahamu kama ni dada yangu wa kuzaliwa tumbo moja kwani jina lake halisi anaitwa Judith Madole na kwamba tangu akiwa bado anaigiza Kaole mimi nilikuwa nikija likizo mjini siku zote nilikuwa nikiishi kwake na kwamba nilihama baada ya kupata mafanikio kwenye muziki,” anasema Marlaw.
Ndiyo kwanza Marlaw anaanza kusimulia katika safu hii, tukutane Jumatatu ijayo kwa mwendelezo wa simulizi yake ya kuvutia sana. Yapo mengi atakujuza kuhusu maisha yake na changamoto alizopitia.
Marlaw: Familia Yetu Ilitengana Baada ya Mama Kufariki
0
November 13, 2019
Tags