MCHEKESHAJI na mshindi wa Shindano la Big Brother 2014, Idris Sultan leo anatarajiwa kuripoti katika Kituo cha Polisi Kati kujua hatima yake baada ya wiki iliyopita kuhojiwa mara mbili mfululizo.
Idris alihojiwa kwa mara ya kwanza Oktoba 31, 2019 ikiwa ni siku moja baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kumtaka Idris kuripoti polisi kwa madai ya kuweka picha yenye sura yake huku akiwa ameketi katika kiti chenye nembo ya Taifa.
Pia, Idris aliweka picha nyingine inayoonyesha sura ya Rais John Magufuli akiwa amesimama huku amevaa suruali yenye mikanda inayoshikizwa mabegani.
Hata hivyo, dakika chache baada ya Makonda kumtaka msanii huyo kuripoti polisi, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla aliahidi kumuwekea dhamana iwapo angekamatwa.
Kutokana na hali hiyo, Idris aliripoti kituoni hapo ambapo alihojiwa kwa saa tano na kupekuliwa nyumbani kwake, hata hivyo usiku aliachiwa kwa dhamana.
Aidha, siku iliyofuata (Novemba Mosi) msanii huyo alihojiwa kwa mara ya pili kwa muda wa dakika 30 na baadaye kutakiwa tena leo.
Kwa mujibu wa mwanasheria wa mchekezaji huyo, Benedict Ishabakaki alisema licha ya kuhojiwa, pia polisi walichukua simu zake kwa uchunguzi zaidi.
“Wamemueleza kuwa kosa lake ni kusambaza habari za uongo chini ya kifungu cha 16 cha sheria ya makosa ya mtandao. Kosa la pili ni kujifanya rais chini ya kifungu cha 15 cha makosa ya mtandao,” alisema.
Aliongeza kuwa alipopekuliwa nyumbani kwake polisi walichukua kompyuta mpakato kwa ajili ya uchunguzi, aliporudishwa kituoni kabla ya kupewa dhamana alipelekwa kitengo cha makosa ya mtandaoni