Mbowe Aiomba Mahakama Apumzike Kutokana na Afya Yake
0
November 26, 2019
Mwenyekiti wa Chama Cha demokrasia na maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe.
Mwenyekiti wa Chama Cha demokrasia na maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe ameiomba Mahakama impe muda aweze kupumzika kutokana na afya yake, ambapo amesema anaumwa homa ya dengue ,malaria na shinikizo la damu.
Mbowe kupitia wakili wake Peter Kibatala ameifahamisha Mahakama hayo leo Novemba 26 mwaka huu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, wakati hiyo ilipokuja kwa ajili ya kuendelea na utetezi.
Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi Novemba 28 mwaka huu itakapokuja tena kuendelea na utetezi.
Katika Kesi hiyo Mbowe na wenzake nane wanakabiliwa na mashtaka 13, ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia na kuhamasisha hisia za chuki.
Mbali na Mbowe wengine wanaokabiliwa katika kesi hiyo, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Salum Mwalimu, Naibu katibu Mkuu bara na Mbunge wa kibamba John Mnyika, mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Kawe Halima Mdee na mbunge wa bunda, Esther Bulaya.
Wengine ni mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko na katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk Vincent Mashinji.
Tags