Mbowe Ashindwa Kuendelea Kujitetea Kisutu
0
November 13, 2019
Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe anayekabiliwa na kesi ya Uchochezi na wenzake katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ameshindwa kuendelea kujitetea kwa sababu mawakili wanaowawakilisha hawakuwepo.
Mbowe alitarajia kuendelea kutoa utetezi wake leo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kupitia mawakili wanaomuongoza lakini hawakuwepo mahakamani.
Katika kesi hiyo ambapo Mbowe anatarajia kuhojiwa na Upande wa Mashitaka, ambapo Wakili wa serikali Mkuu, Faraja Nchimbi amemueleza Hakimu Simba kuwa washtakiwa wote wapo na wapo tayari kwa ajili ya usikilizwaji.
Baada ya kueleza hayo, Wakili wa utetezi Dickson Matata alisimama na kuiieleza Mahakama kuwa anamuwakilisha wakili Peter Kibatala, Prof. Abdallah Safari na Hekima Mwasipu wanaowatetea washtakiwa hao.
Wakili Matata amedai kuwa wakili Kibatala na Wakili Safari hawakufika mahakamani hapo kwa sababu wapo kwenye Kesi Mahakama Kuu ambapo zinasikilizwa Novemba 13 na 14, mwaka huu 2019.
Pia Matata amedai kuwa wakili Mwasipu hakufika mahakamani hapo kwa kuwa amehudhuria kesi inayomkabili Mbunge Suzan Kiwango na wenzake Morogoro leo katika Mahakama ya Wilaya Kilombero Novemba 13 na Novemba 14 mwaka huu.
Matata baada ya kueleza hayo aliiomba Mahakama kuiahirisha Kesi hiyo na kuomba iendelee kusikilizwa Novemba 26 hadi 29, mwaka huu.
Kwa upande wa Wakili Nchimbi, alipinga ombi la kesi kuahirishwa kwa Maelezo kuwa hakuna sababu za Msingi zilizotolewa na upande wa utetezi kuahirisha, pia hawakutoa uthibitisho wowote kuonesha kama ni kweli wapo Mahakama Kuu.
Baada ya Nchimbi kueleza hayo, Wakili Matata akijibu hoja hizo aliieleza Mahakama kuwa hana taarifa za mawakili hao na kuiomba Mahakama itumie busara zake.
Hakimu Simba alisema kwa kutumia busara za Mahakama hatoisikiliza kesi hiyo Novemba 13 na 14 ila kwa kuwa Novemba 15 hakujaelezwa hao mawakili watakuwa wapi hivyo wajulishwe mapema na kwamba kesi itaendelea kusikilizwa tarehe hiyo saa 3 asubuhi.
Katika Kesi hiyo Mbowe na wenzake hao nane wanakabiliwa na mashtaka 13, ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia na kuhamasisha hisia za chuki.
Mbali na Mbowe wengine wanaokabiliwa katika kesi hiyo, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Salum Mwalimu, Naibu katibu Mkuu bara na Mbunge wa kibamba John Mnyika, mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Kawe Halima Mdee na mbunge wa bunda, Esther Bulaya.
Wengine ni mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko na katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk Vincent Mashinji.