Mbunge wa Kawe Halima Mdee, ameingia Bungeni baada ya adhabu yake kuisha leo Jumatatu Novemba 11, 2019, Asubuhi wakati shughuli za bunge zikiwa zinaendelea na kusimamisha shughuli hizo kwa dakika moja alipoanza kusalimia watu na kushangiliwa na Wabunge wa upinzani.
Spika wa Bunge, Jobu Ndugai aliwaonya wabunge wa upinzani wanaomshangilia na kupeana naye mikono ya salamu kuwa watamponza Mbunge huyo.
Kitendo hicho kilimfanya Naibu waziri wa Kilimo, Hussein Bashe ambaye alikuwa anajibu maswali kusimama kwa muda, ili kupisha kelele za wapinzani wakati Mdee akiwa amefika mezani kwa Mbunge wa Vunjo, James Mbatia na kumkumbatia.
Ndugai alitoa onyo kwa msisitizo kuwa makofi ya wabunge wa Upinzani yanaweza kumponza tena Mdee.
“Naomba mtulie, hizo kelele zinaweza kumponza mwenzenu ohoo! si mnanijua….haya shauri yenu” alisema Ndugai.
Kauli hiyo ilimfanya Mbunge Mdee kusimama na kuinama mbele ya kiti cha Spika kuashiria heshima kwa kwa kiti hicho kisha akaketi kwenye nafasi yake na Naibu waziri Bashe akaendelea kujibu swali kwa Waizara yake.
Ikumbukwe kuwa Halima Mdee alikuwa nje ya Bunge baada ya Spika Ndugai kumsimamisha kutokana na kauli yake ya kuunga mkono kauli ya CAG mstaafu Profesa Mussa Asad aliyesema Bunge ni dhaifu.
Kosa ambalo lilimfanya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbles Lema, pia kupata adhabu ya kuwa nje ya Bunge hadi mkutano wa 18 wa Bunge mapema mwakani.
Mdee aingia Bungeni kwa Mbwembwe, Ndugai atoa onyo “si mnanijua”
0
November 11, 2019
Tags