Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amewataka wajumbe wa mabaraza ya Ardhi kuwa makini na watu watakaokuwa wanawasimamia, katika kutatua migogoro na kuleta usuluhishi kwa kuwa mkoa huo, umejaa watu wajanja na wanaojifanya kujua kila kitu.
Hayo ameyabainisha leo Novemba 23, 2019, mara baada ya kuwaapisha wajumbe wa mabaraza ya ardhi ndani ya mkoa huo.
"Mkawe sehemu ya suluhisho na msaada kwa wale akina Mama wajane na kwa watu ambao hawakupata fursa ya elimu, Mkoa huu ni mkoa wa wajanja, matapeli wamejaa hapa na ni mkoa ambao kila mtu ni mjuaji, msipokwenda kutumia busara na hekima mkategemea tu yale yameandikwa kwenye karatasi watu wengi wataumia" amesema Makonda.
Aidha Makonda amewataka wajumbe wa mabaraza ya Ardhi ndani ya mkoa wake, kuhakikisha wanaimaliza migogoro na kutatua changamoto zote za masuala ya Ardhi kwa wananchi na kwamba hategemei kuwaona watu wamejazana kwa Mkuu wa mkoa ama kwa Waziri wa Ardhi na ikiwezekana watoke kuwatafuta watu na kutatua matatizo yao na si kujifungia ofisini.