HATIMAYE Kaimu Kocha Mkuu wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa ameamua kuhamishia kambi ya mazoezi ya timu hiyo kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, baada ya kugundua wachezaji wake wamekuwa wakisumbuka kupata matokeo mazuri wakicheza hapo.
Mkwasa alianza kuiongoza Yanga kwa kupata ushindi wa bao 1-0, katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Ndanda FC, mchezo uliomwezesha kuvuna pointi tatu ugenini, ikiwa ni siku chache tu baada ya kurithishwa mikoba hiyo kutoka kwa kocha wao wa zamani raia wa DR Congo, Mwinyi Zahera.
Habari kutoka ndani Yanga zinasema kuwa Mkwasa ameamua kuhamishia kambi yake ya mazoezi kwenye Uwanja wa Uhuru, ili aweze kujiandaa vizuri na mechi zao zijazo dhidi ya KMC na JKT Tanzania, huku akiachana na Uwanja wa Chuo cha Polisi uliopo Kurasani ambao walikuwa wakiutumia awali kabla ya Zahera kufungashiwa mikoba yake.
“Katika suala la programu za mazoezi kila kocha huwa ana namna yake anavyoamini na ndiyo maana utaona kuwa baada ya Zahera kuondolewa sasa Mkwasa naye ameamua kuuomba uongozi kuhakikisha wanapata nafasi ya kutumia Uwanja wa Uhuru kwenye mazoezi ya kila siku ikianza na michezo miwili ijayo.
“Kwa maana nyingine Mkwasa ameamua kufanya hivyo ili aweze kuwazoea wachezaji wake kutumia uwanja huo, kwani timu ilipokuwa chini ya Zahera ilionekana kupata tabu ya matokeo kwenye inapotumia uwanja huo,” kilisema chanzo.
Kwa upande wa Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli, amekiri kuwepo na mabadiliko hayo, ambapo alisema: “Ni kweli kocha amebadilisha uwanja wa mazoezi na kuanzia leo (jana Alhamisi) timu itafanya mazoezi kwenye Uwanja wa Uhuru hadi mechi zetu za KMC na JKT zitakapochezwa, ila baadaye tutaona wapi tutakapoelekea,” alisema Bumbuli.