Mohamed Salah apigiwa upatu Olimpiki 2020
0
November 22, 2019
Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Misri chini ya umri wa miaka 23 Shawky Gharib, amesema ni mapema mno kutangaza maamuzi ya kumjumuisha mshambuliaji wa Liverpool Mohamed Salah, kwenye kikosi chake kwa ajili ya michuano ya Olimpiki 2020, itakayofanyika mjini Tokyo, Japan.
Tayari Misri imeshafuzu kushiriki michuano hiyo, kwa kutinga hatua ya fainali ya mashindano ya Afrika chini ya umri wa miaka 23, itakayofikia tamati kwa wenyeji kupambana dhidi ya Ivory Coast.
Kanuni za michuano ya Olimpiki zinatoa nafasi kwa kila timu shiriki kuwatumia wachezaji watatu waliozidi umri wa miaka 23, na tayari mashabiki wa soka nchini Misri wameanza kumshawishi kocha Gharib kutomsahau Mohamed Salah.
“Sina budi kujisifia kuwa sehemu ya taifa la Misri, ninapendezwa na kila mchezaji mwenye uwezo wa kuichezea timu yangu, Salah ni mmoja wao, lakini ni mapema mno kusema kama nitamuita kikosini ama nitamuacha, tusubiri muda utakapofika nitafanya maamuzi,” Alisema Gharib.
“Natambua kila shabiki wa soka nchini hapa anataka kuona Mohamed Salah akiwa sehemu ya kikosi cha Misri kitakachokwenda Japan, lakini tukumbuke muda bado ni mrefu mno, tujipe nafasi na kuangalia namna ya kuiwezesha timu kufanya vizuri katika mchezo wa kesho (leo) dhidi ya Ivory Coast, halafu tutaangalia mambo mengine.”
Katika hatua nyingine mshambuliaji wa klabu ya Stoke City Ramdan Sobhi, ambaye kwa sasa anaitumikia Al Ahly kwa mkopo, ameungana na mashabiki wa soka huko Misri kwa kusema, kuna haja ya kocha Gharib kumjumuisha Salah, kwenye kikosi kitakachoshiriki michuano ya Olimpiki 2020.
“Salah anafaa kuwa sehemu ya kikosi kitakachokwenda Japan, na kwa kudhihirisha hilo alinipigia simu na kupongeza hatua ya timu kutinga hatua ya fainali, inadhihirisha anafuatilia kila hatua inayoendelea kwenye fainali za Afrika chini ya umri wa miaka 23, hapa Misri,” alisema Sobhi.
“Najua bado ni mapema mno kuzungumzia nani anapaswa kwenda, na nani hastahili kwenda, lakini dalili za kwenda kupambana zinaanza kuonekana sasa, na sisi tumeshaona Salah ana mchango gani katika soka la kimataifa hivi sasa, hivyo kocha hana budi kumuita ili ajiunge na vijana kwa ajili ya kwenda kulitumikia taifa.”
Kikosi cha Misri chni ya umri wa miaka 23, leo Ijumaa kitakua na shughuli ya kuhakikisha wanabakisha ubingwa wa Afrika katika radhi yao, kwa kucheza mchezo wa fainali dhidi ya Ivory Coast, mchezo ambao utatanguliwa na mpambano wa kumsaka mshindi watatu na wanne kati ya Afrika kusini dhidi ya Ghana.
Michauno ya Olimpiki 2020 imepangwa kuanza kuunguruma mjini Tokyo, Japan kuanzia Julai 24 hadi Agosti 09, huku michuano ya soka ikipangwa kuanza kutimua vumbu kuanzia Julai 22 hadi Agosti 08.
Katika michuano hiyo upande wa wanaume timu kumi na sita zitashiriki, huku wanawake wakitarajiwa kuwa na timu kumi na mbili, kutoka kwenye mabara yote.
Viwanja saba vitatumika kushuhudia miamba upande wa wanaume na wanawake ikimenyana ambavyo ni, National Stadium (Shinjuku,Tokyo), Tokyo Stadium (Chofu, Tokyo), Saitama Stadium (Saitama), Int. Stadium Yokohama (Yokohama, Kanagawa), Ibaraki Kashima Stadium (Kashima, Ibaraki), Miyagi Stadium (Rifu, Miyagi) na Sapporo Dome (Sapporo, Hokkaido).
Tags