Katibu wa NEC ya CCM, Itikadi na Uenezi Humphery Polepole, amesema vyama vya upinzani vilivyokimbia uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 24, mwaka huu, siyo kweli kwamba vilikuwa na nia ya kujitoa ila wameona watapata aibu kutokana na utekelezaji mkubwa wa ilani ya CCM katika mikoa mbalimbali hapa nchini.
Polepole amesema hayo Novemba 17, mwaka huu, kwenye ofisi za CCM mkoa wa Arusha wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya tathimini ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kipindi cha miaka minne tangu mwaka 2015/19 katika sekta mbalimbali.
Amesema kwa mkoa wa Arusha CCM imeridhishwa ba utekelezaji wa ilani ambayo imetekelezwa kwa asilimia 90 katika miradi mbalimbali ya maendeleo.
"Hawa wapinzani wamekimbia uchanguzi wakati mchakato wa rufaa ukiendelea.Kwa kuwa wamekimbia ni vyema wakaendelea na shughuli zinazofanana na kukimbia kwao.Eti wananchi wasubiri maelekezo yenye mwelekeo wa kuvunja amani.Nawambia hivi wasitujaribu," amesema.
Aidha amewaagiza viongozi wa wote wa CCM katika ngazi mbalimbali kwenye mikoa yote ya Tanzania bara inayoshiriki uchaguzi huo kuwaelekeza wananchi kuilinda amani ambayo Mungu ameibariki Tanzania kuwa nayo kwa sababu wananchi ndiyo wa kwanza kusimama katika kulinda amani.
"Vijana wa UVCCM ndiyo walinzi wa Chama.Vijana hao wakae "Standby"kushiriki kikamikifu kuilinda amani sambamba na wale waliopewa dhamana hiyo katika Mamlaka ya Nchi.Hivyo vyombo vya dola visimame katika nafasi yake na sisi CCM tunapenda kutii sheria bila shuruti na inapenda kuona amani ya nchi kitawala muda wote".