Polepole Awavaa Wapinzani..."Wameogopa Upepo wa Kisulisuli"


Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole amesema kuwa watu wa vyama vya upinzani ni waungwana sana kwakuwa wameamua kujitoa wenyewe kwenye mchakato wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, baada ya kukiona chama hicho kilivyo imara na hawawezi kushindana nacho.

 Polepole amesema hayo leo Novemba 13, 2019, Jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na waandishi wa habari.

"Watu wa vyama vya upinzani ni waungwana, wametazama wakasema mambo yatakayotokea kwenye uchaguzi huu si ya mchezo, kwetu sisi ile 2014 inawezekana ulikuwa ushindi wa Tsunami ila wa mwaka huu utakuwa ni ushindi wa kisulisuli na ndiyo maana wakaamua kabla hatujafika pabaya wakaweka mpira kwapani.

“Sisi ndiyo chama pekee wenye ilani ya chama inayotekelezwa, hata katika uchaguzi wa serikali za mitaa tumeandaa ilani ndogo ambayo itakuwa na mambo ambayo tutawaahidi Watanzania na tutayatekeleza,” alisema na kuongeza kwamba  CCM kimeweka  uzito mkubwa katika uchaguzi huu kwa sababu mambo ya maendeleo ya wananchi yanaanzia ngazi ya serikali za mitaa, na ili safu ya uongozi wa juu ikamilike inaanzia chini na safu isipokamilika kunakuwepo na wizi na ubadhirifu katika fedha za umma.

“Chama Cha Mapinduzi tunaingia katika uchaguzi huu tukiwa timamu  ili kupata watu sahihi watakaoweza kumsaidia Mheshimiwa Rais Magufuli kusimamia miradi yetu ya maendeleo na kuijenga nchi yetu.

“Hoja moja ambayo wapinzani wameitoa ni kuwa itungwe kanuni mpya ya uchaguzi.  Sasa tunawauliza wakati tunatunga kanuni hizi pamoja na wao,  walikuwa wamelala?” aliuliza na kuongeza:

“Kitendo cha mtu mzima kama Prof. Lipumba kunitusi na kunibeza kwamba ninaongozwa na njaa ambayo imenipanda kichwani si kitendo cha uungwana hata kidogo, anayejua nina njaa ni mke wangu peke yake na si mtu mwingine.

“Wale wote wanaonituhumu kuwa nimebadili msimamo wa kutetea mambo mbalimbali ikiwemo katiba (ya Warioba) huku wakidai njaa ndiyo imenibadilisha,  nataka niwaambie kuwa sijawahi kukana kauli yoyote niliyowahi kuisema na anayejua kuwa mimi nina njaa ni mke wangu pekee.”

Aidha Polepole amevitaka vyama vya upinzani kujifunza kulingana na historia iliyopita kwakuwa kuna baadhi ya maeneo hawana wafuasi kabisa kama ilivyo CCM.

Hadi kufikia leo Novemba 13, 2019, jumla ya vyama 7 vya upinzani, vimekwishajitoa katika kinyang'anyiro cha Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa kile walichokieleza kuwa hawajatendewa haki baada ya majina ya wagombea wao kuenguliwa.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad