Rais Yoweri Museveni Aingilia Kati Maandamano ya Wanafunzi Chuo Kikuu


Rais wa Uganda, Yoweri Museveni ameagiza wanajeshi wanaozingira chuo kikuu cha Makerere kwa lengo la kutuliza maandamano waondoke mara moja chuoni hapo kwani hiyo sio kazi yao na badala yake jeshi la polisi lisimamie ulinzi chuoni hapo.



Wiki iliyopita, Wanafunzi 15 walikamatwa na Polisi kwa kuchochea vurugu na maandamano wakipinga ongezeko la asilimia 15 ya karo chuoni hapo.



Kwenye maandamano hayo wanafunzi hao walichoma vituo viwili vya Polisi mjini Kampala, Jambo lililopelekea Jeshi liingilie kati ili kutuliza ghasia hizo.



Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa mapema wiki hii na Afisa Habari wa Rais Museveni, Don Wanyama amesema kuwa Museveni ameagiza Wanajeshi waondoke chuoni hapo na jukumu hilo lichukuliwe na Jeshi polisi.



“Rais Museveni kasema wadau na viongozi wa chuo cha Makerere wakae chini kujadili matatizo yanayoendelea katika chuo hicho. Asubuhi hii amempigia Mkuu wa Chuo kamwambia wakae na wenzao wajadiliane. Pia ameagiza Wanajeshi waondoke chuoni hapo na kazi hiyo iwe chini ya Jeshi la Polisi la Uganda,”amesema Wanyama.



Mpaka sasa hatma ya ongezeko la ada chuoni hapo bado haijapatikana, Lakini hali ya usalama imeanza kurejea.



Ongezeko la 15% liliidhinishwa na baraza la vyuo vikuu nchini Uganda, Wanafunzi wanatakiwa kuanza kulipa ada yenye ongezeko hilo kwa miaka mitano ijayo baadaye kila mwanafunzi atatakiwa kulipa 75% zaidi.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad