'Rudisheni Ng'ombe,watoto sio mitaji' - IGP Sirro
0
November 29, 2019
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Simon Sirro, amewataka wazazi wote na walezi mkoani Mara, walioozesha watoto wadogo wakiwemo wanafunzi, kurudisha Ng’ombe walizopokea kama mahari vingenevyo watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.
IGP Sirro ametoa agizo hilo wilayani Bunda mkoani humo, wakati wa uzinduzi wa madawati ya jinsia na kuwataka wazazi wote na walezi, kuhakikisha wanawarudisha watoto wote waliowaozesha na kwamba kama wanataka mali wazitafute kwa kufanyakazi na siyo kufanya watoto wa kike mtaji.
“Baba wa Tanzania hauko juu ya sheria, ukimpiga mkeo ni kosa la jinai, ukimuozesha mwanao kabla ya umri ni kosa utashughulikiwa tu, lazima tufunge watu sasa hata kama wazazi wamekubaliana tutawagonga kwa mujibu wa sheria”amesema IGP Sirro.
Aidha IGP Sirro amelitaka Jeshi la Polisi, kuendelea na kauli mbiu yake ya kutumia nguvu kwa wanaume wote nchini, wanaopiga wake zao ili kukomesha vitendo vya ukatili na kueleza kuwa Mkoa huo ndiyo kinara kwa ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto.
“Bahati mbaya sana mimi ni IGP na natokea Mkoa huu, kuanzia sasa huu ukatili haukubaliki madawati haya ya jinsia yatafanya kazi saa 24, Mama ukipigwa muda wowote wewe nenda kituoni utapata huduma na huyo aliyekupiga atapata huduma anayostahili”ameongeza.
Tags