Serikali yawataka walemavu kusimama na kujipambania
0
November 02, 2019
Serikali imeitaka jamii ya watu wenye ulemavu kusimama na kujipambania katika masuala mbalimbali badala ya kusubiri kuwakilishwa au kupewa nafasi maalum na kwamba itaendelea kuwaelimisha wajihusishe na masuala ya ujasiriamali ili kujiinua kiuchumi.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, anayeshugulikia masuala ya Watu wenye Ulemavu Stella Ikupa hii leo Novemba 1, 2019 katika Kijiji cha Buigiri kilichopo Wilayani Chamwino Mkoani Dodoma wakati akifunga mafunzo ya wajasiriamali Wanawake, Vijana na Walemavu na kuzindua soko lao kibiashara.
Amesema wengi wa walemavu wamekuwa wakisubiri nafasi za upendeleo kitu ambacho si sahihi kwani wanayo nafasi ya kusimama na kupambana katika nyanya mbalimbali za kisiasa, kiuchumi na hata kibiashara kwakua jamii inawaelewa na kuwakubali.
“Mtu mwenye ulemavu hana sababu za kusubiri nafasi za kutengewa maana ana uwezo wa kupambana mfano kama ni siasa simama nadi sera zako utachaguliwa sasa hivi jamii inatambua juhudi za walemavu na hata hizo nafasi za kupewa ni chache jitokezeni,” amehimiza Ikupa.
Hata hivyo Ikupa amewataka wajasiriamali hao kujibidiisha katika kazi ili waweze kumudu uendeshaji wa mitaji waliyopewa na kutimiza masharti ya mikopo waliyoipata kama kianzio katika kujiinua kibiashara na kufanikisha ndoto walizojiwekea maishani mwao.
Awali akiongea katika eneo hilo mbunge wa Jimbo la Chilonwa Joel Mwaka amesema Setikali inaangalia kwa ukaribu matatizo ya Wananchi na kutoa shukrani zake kwa mgeni rasmi Naibu Waziri Ikupa kwa kuona umuhimu wa kuhimiza masuala ya uwajibikaji kwa walemavu.
Amesema licha ya kuendelea na uelimishaji wa masuala ya kiujasiriamali pia walemavu wanatakiwa kuwa wabunifu katika kuzalisha na kuuza bidhaa na kwamba wananchi wasiwafiche watu wenye ulemavu kwani wanao uwezo wa kupambana huku akizishukuru taasisi za TAKUKURU, benki ya NMB na Serikali kwa kuwezesha mafunzo hayo.
“Tusiishie kuwaficha walemavu ndani, tuwatoe wanao uwezo wa kupambana lakini pia tuwashukuru wadau wawezeshaji ambao wamefanikisha mchakato huu tangu mwanzo huu ni mfano wa kuigwa na watu wengine wenye kupenda maendeleo, “Ameongeza Mbunge Mwaka.
Kwa upande wake mjasiriamali na Mkurugenzi wa Taasisi ya Nakua na Taifa langu Jessica Mshama amesema mafunzo hayo ya ujasiriamali ni ujio bora elimu kwa vinaja, akina mama na walemavu katika kujitambua na kujiinua kiuchumi na kwamba jamii inatakiwa kuwaunga mkono kwa kununua bidhaa zao.
Naye Afisa mahusiano wa benki ya NMB tawi la Chamwino Emil Mrumah amesema tayari wajasiriamali hao wamejifunza na sasa wanaenda kutenda ili wawe na maisha bora na kuwahimiza kutumia vyema fedha walizowezeshwa ili wazirejeshe na kuwakopesha wengine.
Tags