Soma Kisa Hichi Cha Mama Aliyeibiwa Pochi na Simu Kwenye Daladala......


Wakati naanza kazi, nilifurahi sana wakati wa mshahara na nilikuwa na mengi ya kufanya. Nilihitaji geto lipendeze, nivae nguo safi niwe sawa na wengine. 

Basi, mwisho wa mwezi mshahara ukaingia kwene account. Nilipanga kwenda kununua vitu vingi vya geto na nguo kidogo. Nikaondoka, nikapanda gari za Kariakoo.

Tulipofika pale Tegeta kwa Ndevu, akaingia mama mmoja mtu mzima. Kavaa vizuri anaonekana mama mstaarabu. Nikaona ngoja nimpishe kiti akae. Nikasimama. Alinishukuru, akakaa. 

Basi tulipofika pale Lugalo, konda akaanza kudai nauli. Akafika kwa yule mama, ghafla ugomvi ukaanza. Masikini yule mama alilalamika haoni walet yake, na pochi imechanika.

Konda akawa mkali, akimrushia yule mama maneno. Yule mama alikaa kimya... Kwa aibu na fedheha. Konda akasema, utashukia hapo ITV. Yule mama akasema, nitashuka hakuna shida. Kondakta akaendelea kukusanya kwa wengine huku akimwita yule mama Tapeli.

Watu wengi waliongea, na kusema kuwa matapeli wamekuwa wengi siku hizi. Wengine walimtetea yule mama na kusema konda amasamehe. Yule mama, akasema nimeibiwa jamani, na simu yangu pia siioni ndio maana nakuwa mpole. Watu wakazidi kulumbana.

Konda akafika kwangu, nikamwambia nalipa na ya yule mama. Akaropoka “mama kuna mtu kakuokoa” basi yule mama akakaa kimya. Tulipofika Kariakoo,tukashuka. Yule mama akaja akaniambia “Asante mwanangu”.

Akaendelea kusema, mwanangu nimeibiwa vitu vyangu pamoja na simu pia. Sijui vimechukuliwa saa ngapi. Nilikuwa na lengo la kuja kumnunulia mwanangu viatu na madaftari anaenda shule wiki ijayo.

Pamoja na kupata wasiwasi na moyo kusitasita... Bado huruma ilinijaa baada ya kusikia yaliyomkuta mama yule. Naelewa jinsi wazazi wanavyopambana kwa ajili ya watoto. Mimi nilishuhudia wazazi wakiuza mali zao nisome. Hivyo nilielewa.

Nikamwambia mama, pole sana. Sasa mimi mwanao sina pesa nyingi ila chukua hii elfu 50. Kamhudumie mwanao. Nilikuwa naweza kumpa zaidi, ila nikatoa kwa akili, kama ni wizi basi nipigwe kidogo kama ni baraka zitarudi. Mama alinishukuru sanaaa.

Akasema “MUNGU wa mbinguni, aliyeiumba dunia akubariki,  uzao wako ukawe wa faida... Kazi zako zikawe na faida... Mapato yako yakajae kwa wingi... Milango ya mbinguni ikufungukie... MUNGU yeye Jehova akupe afya tele” moyo wangu ulijaa furaha.

Nilisikia amani na kumwambia yule mama “Amen, asante mama Yangu” basi akaniambia jina lake. Akanipa namba yake. Akasema akirenew line, tutawasiliana. Niwe najaribu kumcheki. Miaka ikapita. Nikawa mtu mzoefu kazini. Nimefanikiwa kiasi kikubwa. Nimenunua ndinga. Maisha yanaendelea.

Mwaka Huu, mwezi wa 10. Nikaona kazi zimetangazwa katika shirika kubwa. Na wanataka coordinator, mtu mwenye uzoefu. Nikaomba ile kazi. Nikawa nasubiri majibu. Baada ya wiki 3, wakanipigia simu. Kwamba kuna usaili..natakiwa kufika.

Siku ya usaili, nikawahi mapema. Walisema saa mbili, mimi nikafika saa moja na nusu. Nikapokelewa, nikakaa mapokezi kwenye viti vya wageni. Ghafla akaingia mama mmoja safi, kavaa kibosi, kwa kweli alikuwa na muonekano wa Kibosi. Akaomba kitabu cha mahudhurio. Nilivyomwona....nikaanza kuhisi namfahamu. Nikawa nawaza. Akafika pale akanisalimia, nikasimama nikampa mkono.

Akanisalimia kwa uchangamfu, huku Akitabasamu. Akaniuliza, “Are you here for the interview? ” nikamjibu “Yes madam I'm ”. Akasema, You're welcome, and all the best. 

Nikasubiri, muda ukafika ingawa walichelewa sana kutuita kuingia kwenye usaili. Nikahojiwa na wazungu waliotoka CDC na wabongo pia walikuwepo. Mwisho,  wakasema "our director for Administration and Finance has strongly recommended you for the job".

She is a very efficient woman and we trust her. So, if she recommendes you,  we believe you're worthy. Basi, nikapata ile kazi. Nikasema lazima nimuone huyo mama, nimshukuru.

Kufika, msaidizi wake akanipeleka mpaka kwenye ofisi yake. Yule mama akaniita "Stephen mwanangu karibu ". Akaniuliza "unanikumbuka? " nikasema mama hapana. Akanielezea kisa kile cha miaka ya nyuma. Akasema wakati ule alikuwa anasoma hapo open university Masters yake, Lakini maisha yalikuwa magumu sana. Na alikuwa na watoto. Lakini, akapata kazi nzuri.

Akakumbuka wema wangu. Maana kumbe yeye alikuwa na elfu 30. Ikaibiwa, mimi nikampa 50. Akasema aliahidi, kuwa MUNGU akimpa nafasi atalipa wema ule. 

Tutende wema kwa kuangalia utu na ubinadamu. Tujifunze kuona mema kwa wenzetu sio mabaya. Tuwahi katika kila jambo twende na muda.” - Steven Msangi, Dar Es Salaam.  #WatuNiStory

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad