Taifa Stars Yapigwa na Libya 2-1, Samatta Atupia


MWAMUZI wa mchezo wa jana kati ya Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars dhidi ya Libya wa kuwania kufuzu Afcon 2021 nchini Cameroon, aliiua Tanzania bila huruma kwa kuipa Libya penalti ya utata.



Mchezo huo uliochezwa usiku wa kuamkia leo kwenye Uwanja wa Olympique Mustapha Ben Jannet Monastir hapa Tunisia, ulianza kwa kasi kubwa na Stars ilianza kuandika bao la kwanza dakika 18 kupitia kwa nahodha, Mbwana Samatta akifunga kwa mkwaju wa penalti baada ya Simon Msuva kuangushwa kwenye eneo
la hatari. Kipindi cha kwanza kilimalizika kwa Stars kuwa mbele kwa bao 1-0.


Kipindi cha pili, mwamuzi aliipa Libya penalti dakika ya 66 kwa kile alichotafsiri mpira ulimgonga mkononi beki wa Stars, Bakari Mwamnyeto huku picha za video zikionyesha mpira huo ulimgonga beki huyo kwenye goti. Sand Masaud akafunga penalti hiyo.



Bao la pili la Libya lilifungwa na Anis Mohamed Saltou dakika ya 80 baada ya safu ya ulinzi ya Stars kushindwa kuokoa hatari. Zikiwa zimesalia dakika tatu kabla ya kufika tisini, Libya walipata pigo baada ya Hamdou El Houni kuonyeshwa kadi ya pili ya njano iliyoambatana na nyekundu na kutolewa uwanjani.


Hadi mwisho wa mchezo huo wa Kundi J, Libya waliibuka na ushindi huo na kupata pointi tatu za kwanza baada ya mechi ya awali kufungwa 4-1 na Tunisia. Stars iliyoanza kwa ushindi wa 2-1 dhidi ya Equatorial Guinea, imesalia na pointi zake tatu. Mchezo mwingine wa kundi hilo uliozikutanisha Tunisia na Equatorial Guinea, hadi dakika ya 79, Tunisia ilikuwa mbele kwa bao 1-0

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad