Vyama vya msingi Kagera vyapata neema kutoka Benki ya TADB
0
November 18, 2019
Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imekabidhi Pikipiki mpya mbili Kwa vyama viwili vya msingi vya Ruicho na Nyakatuntu vya Wilayani Karagwe na Kyerwa mwishoni mwa Wikiiliyopita, katika Hafla fupi iliyofanyika katika Ukumbi wa Chama cha Ushirika KDCU Wilayani Karagwe.
Awali akitoa salaamu za Benki hiyo Meneja wa TADB Kanda ya Ziwa, Mike Granta kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji, Japhet Justine, amesema TADB kupitia mkopo inayotoa Kwa wakulima, imekuwa na mchango mkubwa wa maendeleo kwa Mkulima mmoja mmoja na pamoja na Vyama vya msingi, huku akiongeza kuwa mpaka sasa zaidi ya shilingi Bilioni 44 ambazo zimeingia katika mzunguko wa kiuchumi shilingi Bilioni 34, kati ya pesa hizo zikiwa tayari zimelipwa kwa Wakulima wa Wilaya za Karagwe na Kyerwa.
Kupitia Hafla hiyo Meneja Granta amekabidhi Jumla ya Pikpiki mbili mpya zenye jumla ya thamani ya Shilingi Milioni Tano, ikiwa ni ahadi iliyotolewa hivi Karibuni na Mkurugenzi Mtendaji Japhet Justine alipofanya ziara yake Wilayani Karagwe, Sababu kubwa ikiwa Vyama hivyo kufanikisha zoezi la kuwashawishi na kuwaunganisha pamoja wanachama wao kwa asilimia kubwa kufungua akaunti katika Benki hiyo.
Mgeni Rasmi katika hafla ya kukabidhi Pikipiki hizo Mkuu wa Mkoa Kagera Brigedia Jenerali Marco Gaguti akizungumza na Wakulima hao, amesema kwa Upande wa Serikali mpaka sasa hali ni shwari kwa msimu huu wa ukusanyaji wa kahawa, Amani na Utulivu ni vyakutosha kulinganisha na msimu uliopita, hali iliyochangiwa na ulipaji wa malipo yote ya awali kwa wakulima wa zao hilo, na kwamba hakuna mkulima yeyote anayedai.
Aidha Gaguti ameongeza kuwa hakuna mnunuzi aliyezuiliwa kununua kahawa kutoka Kagera, Bali wanunuzi wa kahawa ya msimu huu kwa asilimia mia moja ni wanunuzi binafsi, na wale wachache wanaolalamika na kueneza uzushi ni wale ambao hawakukidhi vigezo vya kibiashara, na ndio sababu msimu huu umekuwa bora kuliko misimu iliyopita.
Tags