Waliotumia JINA la Mke wa Rais Magufuli Kutapeli Wahukumiwa
0
November 07, 2019
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewahukumu watu wanne kulipa faini ya Sh1.5 milioni kila mmoja baada ya kuwatia hatiani kutumia jina la Janeth Magufuli, mke wa Rais wa Tanzania John Magufuli kutapeli Sh4.4 milioni.
Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewahukumu watu wanne kulipa faini ya Sh1.5 milioni kila mmoja baada ya kuwatia hatiani kutumia jina la Janeth Magufuli, mke wa Rais wa Tanzania John Magufuli kutapeli Sh4.4 milioni.
Wanadaiwa kujipatia kiasi hicho cha fedha kwa njia ya udanganyifu baada ya kufungua ukurasa katika mtandao wa kijamii wa Facebook kwa jina la Janeth Magufuli.
Mbali na faini hiyo, mahakama hiyo imetaifisha gari aina ya Toyota Raum pamoja na simu nane vilivyotumika katika utapeli huo.
Waliohukumiwa kulipa faini hiyo ni Saada Uledi, Maftaha Shabani, Heshima Ally na Shamba Baila.
Hukumu hiyo imetolewa leo Jumatano Novemba 6, 2019 na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Huruma Shaidi baada ya washtakiwa hao kutiwa hatiani katika mashtaka mawili kati ya manne yaliyokuwa yanawakabili.
Washtakiwa hao walikiri makosa yao na kuingia makubaliano na mkurugenzi wa mashtaka nchini (DPP).
Washtakiwa hao wanadaiwa kati ya Januari 2017 na Machi mwaka huu katika jiji la Dar es Salaam walikula njama kwa kuchapisha taarifa za uongo kupitia akaunti yao ya mtandao wa kijamiii ya Facebook.
Inadaiwa kuwa siku hiyo ya tukio, washtakiwa walichapisha machapisho katika akaunti yao ya mtandao wa kijamii wa Facebook wakionyesha kuwa Janeth ameunda taasisi ya kukopesha na kutoa mikopo kwa watu mbalimbali ikiwa na masharti ya kuweka fedha kabla ya kupewa mkopo kamakinga ya mkopo, huku wakijua kuwa ni uongo.
Pia wanadai Machi 2 na 8, 2019 katika jiji la Dar es Salaam, wakiwa kama waendeshaji wa akaunti hiyo ya Facebook, walisajili akaunti kwa jina la Janeth Magufuli kwa nia ya kudanganya na kujipatia Sh 4,487,000 kutoka kwa Paul Kunambi kama kinga ya mkopo, wakati wakijua kuwa sio kweli.
Katika shtaka la utakatishaji wa fedha, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kuwa kati ya Machi 2 na 8, 2019 walijipatia Sh 4, 487,000 huku wakijua kuwa fedha hizo ni zao la fedha haramu zilizotokana na udanganyifu
Tags