Yanga Kuwapa Wachezaji Wao Toyota Crown Mpya
0
November 13, 2019
YANGA mambo ni moto! Unaambiwa kuwa kama itafanikiwa kushinda mechi zake 36 walizobakisha msimu huu wa Ligi Kuu Bara, basi kila mchezaji atamiliki gari aina ya Toyota Athlete Crown yenye thamani ya Sh Mil.13 atakalotanua nalo mtaani mwishoni mwa msimu.
Yanga hadi hivi sasa tayari imecheza michezo mitano ya ligi, kati ya hiyo mmoja imepoteza kwa kufungwa na Ruvu Shooting bao 1-0, kabla ya kutoka sare ya mabao 3-3 na Polisi Tanzania.
Ukiachana na michezo hiyo miwili, Yanga imeshinda michezo mitatu ya ligi dhidi ya Coastal Union, Mbao FC na Ndanda FC ambazo zote zilipata ushindi wa bao 1-0 kwenye kila mchezo.
Yanga ilianza kupata ushindi katika michezo hiyo ya ligi baada ya wadhamini wao Kampuni ya GSM ambao ndiyo watengenezaji wa jezi zao za msimu huu kuwawekea dau la Sh Mil. 10 kwenye kila mchezo watakaoshinda kabla ya kuanza kupata ushindi wao wa kwanza walipocheza na Coastal.
Wachezaji hao watanunua magari hayo kutokana na fedha hizo wanazopewa baada ya kushinda michezo yote ya ligi na mwishoni mwa msimu.
Mastaa hao ili watanue na magari hayo wanatakiwa kushinda michezo 36 wanayoendelea kuicheza ya ligi baada ya kupoteza miwili pekee na kama wakishinda yote basi mwishoni mwa msimu watakuwa wamejikusaniya Sh Mil. 360 jumla.
Baada ya kupata Sh Mil. 360, kila mchezaji atapata mgawo wa Sh Mil. 13 kati ya wachezaji 27 waliosajiliwa kwenye msimu huu wa ligi ambazo zitatosha kabisa kununua gari mpya aina hiyo ya Crown mwishoni mwa msimu.
Hata hivyo, wachezaji hao wa Yanga huenda wakapata fedha kubwa kutoka kwa GSM kama wakifanikiwa kuwafunga watani wao wa jadi, Simba watakapokutana mara mbili kwenye mzunguko wa kwanza na wa pili katika msimu huu na wanaweza kumaliza msimu kwa kukusanya zaidi ya Sh Mil. 14.
Hali kama hiyo, waliifanya GSM wakati Yanga ilipocheza michezo yake miwili ya Kombe la Shirikisho Afrika walipokutana na Pyramids FC ya Misri ambapo walitoa ahadi ya Sh Mil. 30 kama wangefanikiwa kuwaondoa wapinzani hao.
Simba na Yanga zinatarajiwa kuvaana Januari 4, mwakani katika mchezo wa raundi ya kwanza wa ligi unaotarajiwa kupigwa kwenye Uwanja wa Taifa
Tags