Waziri awapa neno viongozi waliopita bila kupingwa
0
November 26, 2019
Serikali imejipanga kuimarisha sekta ya kilimo ikiwa na dhamira ya kumkomboa mkulima kwa kuimarisha masoko ya bidhaa zao sambamba na kuimarisha upatikanaji wa pembejeo za uhakika na kwa wakati.
Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga akizunguma na viongozi wa CCM waliopita bila kupingwa.
Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga, amesema hayo jana Novemba 25, 2019, wakati akizungumza na wenyeviti wa Chama cha Mapinduzi waliopita bila kupingwa, katika jimbo la Vwawa mkoani Songwe.
Waziri Hasunga amesema endapo wakulima watafuata maelekezo ya wataalamu mbalimbali wa kilimo, wataongeza uwezekano mkubwa katika uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara, jambo litakalopelekea kuimarisha kipato cha mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
"Waambieni wakulima wote wawe wanatunza mifuko ya mbegu wanazonunua ili ikionekana hazijaota sisi tushughulike na wote wanaosambaza, hata shetani alipoasi, Mungu alimtupa duniani pamoja na kwamba alikuwa muimbishaji mkuu wa kwaya ya mbinguni" amesema Waziri Hasunga.
Katika hatua nyingine Waziri Hasunga amepiga marufuku wafanyabiashara kwenda vijijini na debe la kupimia mazao, badala yake wanapaswa kufuata utaratibu sahihi wa kutumia vipimo vinavyotakiwa ambavyo ni Mizani za Kidigitali.
Aidha Waziri Hasunga amesema kuwa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa umemalizika hivyo amewataka wenyeviti hao, kuvunja makundi yote yaliyotokana na uchaguzi ili wananchi wote washiriki shughuli za maendeleo na kutekeleza kwa ufasaha ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2015/2020.
Tags