Waziri Mkuu aagiza Mkurugenzi Mtwara kuchukuliwa hatua


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema mtu yoyote anayekwaza wawekezaji nchini atachukuliwa hatua kali, hivyo amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Gelasius Byakanwa amchukulie hatua Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mtwara, Bw. Maisha Selemani Mtipa baada ya kumtaka mwekezaji alipe sh. milioni 31.6 kwa ajili ya gharama za vikao ili aweze kupatiwa eneo.

Ametoa agizo hilo, wakati akifungua Kongamano la Uwekezaji na Maonesho ya Biashara mkoa wa Mtwara lililofanyika kwenye Viwanja vya Chuo cha Ualimu Mtwara. “Yoyote anayekwaza uwekezaji nchini kwa kuwasumbua wawekezaji tutamshughulikia kabla ya kuwasumbua wawekezaji.”

Amesema Bw. Mtipa amemwandikia barua mwekezaji wa kampuni ya MBR Internation Company Limited akimtaka alipe sh. milioni 31.6 kwa ajili y a kulipa kamati mbalimbali zikiwemo sh. milioni 1.95 kwa kamati ya Menejimenti ya Halmashauri.

Waziri Mkuu amesema “fedha nyingine sh. milioni 2.27 kwa kamati ya kugawa ardhi ya wilaya, sh. milioni 4.43 kamati ya Uchumi Ujenzi na Mazingira, Kamati ya Fedha, Utawala na Mipango sh. milioni 5.14 na sh milioni 17.79 Baraza la madiwani ili wagawane tu, huu ni utaratibu wa wapi? huku ni kufukuza na kukwaza wawekezaji.”

Waziri Mkuu amesema Serikali imeshaondoa tozo zaidi ya 150 zilizokuwa zinakwaza wawekezaji kupata uwekezaji katika maeneo mbalimbali nchini, hivyo haitaki kusikia mahali popote panawekwa tozo zenye kuwakwaza wawekezaji. Amesema hatua zitakazochukuliwa kwa Bw. Mtipa ziwe fundisho kwa halmashauri zote nchini.

Mapema, Waziri Mkuu alizungumzia uuzwaji wa korosho na kuagiza kwamba mfumo uliotumika katika mnada wa kwanza wa uuzwaji wa zao la korosho uliofanyika jana (Alhamisi, Oktoba 31, 2019) ndio unaopaswa kuendelea, hivyo ameagiza wahusika wausimamie vizuri ili usiingie dosari.

Alisema Serikali ilibaini changamoto katika uuzwaji wa mazao mengine ya pamba na kahawa ya uwepo wa watu ambao wananunua mazao nje ya mfumo kama kangomba, hivyo ni muhimu wakadhibitiwa ili fedha zote ziende kwa wakulima.

Pia Waziri Mkuu aliagiza maandalizi yawe yanakwenda pamoja na msimu kama suala la magunia wasiachiwe watu wa ushirika pekee bali Wakuu wa Mikoa na Wilaya nao washiriki katika kutatua tatizo hilo ili minada ifanyike kikamilifu.

Pia chama kikuu cha ushirika pamoja na vyama vya msingi wazuie kuwepo kwa makato ya hovyo ambayo yalishaondolewa na Serikali ili kuhakikisha mkulima haumizwi kwa kupunguzwa kwa malipo yake.

Amewataka viongozi hao wasimamie mtiririko wa fedha kutoka kwa wafanyabiashara kwenda kwa mkulima na wahakikishe zinaingizwa katika akaunti za wakulima. Pia sheria ya ununuzi isimamiwe baada ya mnunuzi kupewa zabuni anatakiwa alipe ndani ya siku nne. “Sheria hii itaondoa watu wa kati na kumwezesha mkulima kulipwa fedha zake kwa wakati.”

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa amesema amesema wanunuzi wote wametakiwa wahakikishe wakulima wanalipwa kwa wakati. “Bei ya chini katika mnada wa korosho uliofanyika Mtwara ilikuwa sh. 2,409 na bei ya juu ilikuwa 2,559 na hali inaonesha uhitaji wa korosho duniani ni mkubwa kutokana na ubora wake.”

Amesema chama cha ushirika cha TANECU waliingiza sokoni tani 13,000 huku mahitaji yakiwa ni tani 40,000 na chama cha ushirika cha MAMCU walipelela sokoni tani 7,000 na mahitaji yalikuwa tani 22,000 hivyo wafanyabiashara wengi jana walikosa korosho.

Akizungumziakuhusu kilimo cha zao la korosho, Waziri Mkuu ametoa rai kwa viongozi wa mkoa wa Mtwara kuwa wasibweteke kwani mikoa mingine nayo imeanza kulima korosho, hivyo waweke mikakati mizuri ili zao la korosho liendelee kuwa zao kuu la biashara kwa mkoa.

Amesema Serikali kwa upande wake, itaendelea kuweka mazingira rafiki na miundombinu wezeshi kwa ajili ya kuvutia wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza mkoani Mtwara.

 “Tusisahau kuwa Mkoa wa Mtwara ni korosho na korosho ndiyo mkoa. Hili linadhihirishwa na usemi wa wenyeji kuwa korosho ni dhahabu ya kijani. Mtwara ndiyo mzalishaji mkubwa wa korosho Tanzania, huzalisha zaidi ya asilimia 65 ya korosho zote nchini.”

Kadhalika, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwaasa wawekezaji wote kwamba waondoe hofu kuhusu kuwekeza Mtwara kwa sababu mkoa wa Mtwara wa sasa ni tofauti na Mtwara ile waliyokuwa wanaisikia zamani, uchumi wake unakuwa.

Waziri Mkuu amesema ushiriki wao kwenye kongamano hilo unaonesha utayari walionao katika kuiunga mkono Serikali kwa lengo la kuwaletea maendeleo na kujenga Tanzania ya Uchumi wa Viwanda ambayo wote wanaitamani.

Kongamano hili na mengine yaliyofanyika kwenye mikoa mbalimbali ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu alilolitoa wakati anafungua Kongamano la tatu la uwezeshaji wananchi kiuchumi jijini Dodoma Juni 18, 2018, ambapo aliagiza mikoa yote kuandaa Mwongozo wa Uwekezaji wa Mkoa.

“Niendelee kusisitiza tena kwa mikoa ambayo bado haijatekeleza agizo hili la kuandaa Mwongozo wa Uwekezaji ifanye hivyo mapema.”

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema licha ya Serikali kuwekeza kwa kiwango kikubwa kwenye miradi ya kijamii katika Mkoa wa Mtwara, pia imewekeza kwenye miradi mikubwa ya kimkakati ambayo inachochea kukua kwa uchumi kwa haraka.

Waziri Mkuu ameitaja miradi hiyo ni pamoja na upanuzi wa uwanja wa ndege na bandari ya Mtwara; ujenzi wa barabara ya lami kutoka Mtwara hadi Nanyumbu mpakani na Msumbiji; ufufuaji na ujenzi wa viwanda vya kubangua korosho.

Miradi mingine ni ujenzi wa reli kutoka Mtwara hadi Songea kwa ajili ya kusafirisha makaa ya mawe kutoka Mchuchuma na chuma kutoka Liganga na kuongeza uzalishaji wa umeme kwa kutumia gesi asilia na vyanzo vingine.

Ufunguzi huo umehudhuriwa na Waziri wa Nchi - Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Angellah Kairuki, Waziri wa Kilimo Josephat Hasunga, Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa,Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme na watendaji wengine wa Serikali
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad