Waziri wa Katiba na Sheria Aitaka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kuimarisha utawala bora


Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Dkt. Augustino Mahiga ameitaka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) kuimarisha misingi ya utawala bora nchini ili kuboresha utoaji wa huduma za Serikali kwa jamii.

Waziri Mahiga alitoa kauli hiyo Novemba 18, 2019 jijini Dodoma katika kikao kilichofanyika kwenye ofisi za Wizara ya Katiba na Sheria baina yake na Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mheshimiwa Mathew Mwaimu.

Akiongea katika kikao hicho, Waziri Mahiga alieleza kuwa tume ni chombo muhimu ambacho kimepewa mamlaka ya kusimamia mambo mawili ambayo ni  haki za binadamu na utawala bora.

Waziri Mahiga aliendelea kusema  kuwa tume katika kipindi chote cha utekelezaji wa majukumu yake imekuwa ikifanya kazi kubwa katika masuala ya haki za binadamu zaidi ya utawala bora, na hivyo, kuwataka katika awamu hii ya tano wawekeze nguvu zaidi katika kuimarisha misingi ya utawala bora.

“Tume ni chombo muhimu katika kujenga ustawi wa jamii, hususani kujenga jamii yenye utamaduni wa kuheshimu haki za binadamu nchini, lakini msisahau kujenga utawala bora”, alisema Mahiga

“Mheshimiwa Rais anaposema serikali hii ni ya wanyonge, anataka wale watu walio kwenye mamlaka walijue hilo na wazingatie utawala bora katika kuhudumia jamii, na nyie ndio wenye jukumu la kuhakikisha misingi ya utawala bora inaimarika nchini”aliongeza Maiga

Katika hatua nyingine Waziri Mahiga aliitaka tume kuieleza na kuifafanulia jamii utekelezwaji wa haki za binadamu  unavyotekelezwa kwa vitendo na serikali ya awamu ya tano.

Mahiga alisema pamoja na changamoto zinazopigiwa na kelele na wadau wa masuala ya haki za binadamu, lakini ni ukweli uliowazi kuwa serikali ya awamu ya tano imetekeleza na inaendelea kutekeleza haki mbalimbali kwa vitendo na kuhakikisha haki hizo wananchi wanazipata.

Alieleza kuwa serikali ya awamu ya tano imetekeleza kwa vitendo haki ya kupata elimu kwa kutoa elimu bure kwa wanafunzi kuanzia shule za msingi mpaka sekondari.

Pia, alieleza kuhusu haki ya afya ambapo wazee wameanza kupata matibabu bure, na upatikanaji wa bima ya afya kwa wananchi.

“Hizi jitihada zote za serikali katika kuwapatia huduma wananchi bado hazijaelezwa vya kutosha, tume tumieni nafasi yenu kuyaeleza haya kwa jamii iweze kuelewa”alisisitiza Mahiga

Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Profesa Sifuni Mchome alimueleza Mwenyekiti wa tume kuwa masuala ya haki za binadamu yanafanywa na taasisi nyingi na hivyo kipindi hiki wawekeze nguvu zao katika kuimarisha utawala bora na utawala wa sheria nchini.

“Tume ni lazima muonekane mnachukua hatua, wekeni mkakati wa viashiria vya kubaini haraka changamoto  zinazoelekea kuathiri utawala bora na kuzifanyia kazi”, alisema Mchome

Akizungumza mapema, Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala bora, Mheshimiwa, Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu alimueleza Waziri Mahiga dhamana waliyopewa wataitumia vyema katika kusaidia serikali kutimiza lengo lake la kuifikisha nchi katika uchumi wa kati.

“Tume itaendelea kuunga mkono jitihada za serikali na tutatekeleza majukumu yetu kwa kuzingatia taratibu, sheria na katiba ya nchi”alisema Mwaimu

Mwenyekiti huyo wa Tume alikwenda kutembelea Wizara ya Katiba na Sheria kwa lengo la kujitambulisha kwa Waziri Mahiga ikiwa ndio mara yake ya kwanza tangu alipoapishwa Novemba 4, 2019.

Katika ziara hiyo Mwenyekiti aliongozana na  Makamu Mwenyekiti, Mohamed Khamis Hamad, na Makamishna wengine watano ambao ni  Mheshimiwa, Dkt. Fatma Rashid Khalfan, Mheshimiwa Thomas Masanja, Mheshimiwa Amina Talib Ali, Mheshimiwa Khatib Mwinyi Chande  na Mheshimiwa Nyanda Josiah Shuli.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad