WHO yawaondoa wafanyakazi wake eneo la Biakato DRC


Kufuatia mashambulizi ambayo yamefanywa na waasi katika eneo la Biakato nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, shirika la Afya la Umoja wa Mataifa WHO limeamua kuwaondoa wafanyakazi wake eneo hilo.

Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa WHO linawaondoa sasa wafanyakazi wake Biakato na kuwapeleka Beni katika mkoa jirani wa Kivu ya kaskazini. Wakati huko hali ikiwa hivyo, mkuu wa majeshi ya Congo yuko ziarani katika mji wa Beni kutathmini hali ya operesheni ya kupambana na waasi katika eneo hilo.

Kwa mjibu wa wakaazi wa Biakato, mchana wa leo, milio ya risasi ilikuwa ikisikika katika mji huo na lakini haikujulikana kwanini kwani, jeshi la serikali lilikuwa tayari limewafurusha wapiganaji wa maimai walio wauwa wafanyakazi wa shirika la afya Ulimwenguni WHO toka mji huo.

Akizungumza na DW, naibu mwenyekiti wa baraza la vijana wa Biakato, Kabuyaya Saidi akitupatia hali inayojiri Biakato wakati huu, anasikitika pia kuona WHO inawaondoa wafanyakazi wake toka Biakato, wakati kuna wagonjwa watatu wa Ebola katika maeneo aliyoyataja.

Gari la Umoja wa Mataifa likiteteketea Beni baada ya kuwashwa moto na waandamanajiGari la Umoja wa Mataifa likiteteketea Beni baada ya kuwashwa moto na waandamanaji
Aidha Kabuyaya Saidi aliwatahadharisha wapiganaji wa maimai wanaozorotesha usalama katika mji mdogo wa Biakato pamoja na viunga vyake, pale akihofia maambukizi mapya ya EBOLA, watabibu karibia wote wakiwa wameondoka mjini humo.

Kwa upande wake naibu mwenyekiti wa shirika la kutetea haki za binaadamu CEPADHO Omar Kavota, naye anahofia maambukizi mapya, aliliomba shirika la afya Ulimwenguni WHO kusimamisha hatua ya kuwaondoa wafanyakazi wake Biakato kwani, huenda mashirika mengine ya afya yakawaondoa pia wafanyakazi wao katika maeneo mengine.

Wakati  huo  huo ,Mkuu wa majeshi ya Congo generali Mbala Musense, yuko ziarani katika mji wa Beni,

akiwa ameandamana na magenerali wengine wa jeshi la Congo. Madhumuni ya ziara yao hapa ni kutathmini hali ya mambo inayojiri hapa,pamoja na kukadiria operesheni kabambe dhidi ya ADF, waasi kutoka Uganda, inayoendelea katika viunga vya mji wa Beni, pamoja na maeneo ya vijiji vya wilaya ya Beni.

Ujumbe kabambe huo wa jeshi la serikali unawasili Beni, wakati raia wanalalamikia mauwaji ya kila uchao katika viunga vya mji wa Beni, pamoja na maeneo ya wilaya ya Beni ambako operesheni kabambe dhidi ya ADF bado kuanzishwa.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad