Wizkid Ayo amepanga kuiweka Tanzania kwenye mradi wake mpya wa muziki akitumia mazingira, warembo na watalaam kutoka ‘ardhi ya Nyerere’.
Mkali huyo wa ‘Joro’ ambaye jana alikuwa miongoni mwa wasanii waliopanda kwenye jukwaa la Wasafi Festival jijini Dar es Salaam, amesema kuwa atarekodi video ya wimbo wake mpya kabla hajarudi nchini Nigeria.
“Nitafanya video ya wimbo wangu nikiwa hapa, na nitafanya na muongozaji anaitwa Kenny. Itakuwa video maalum na nitakuwa na wasichana maalum kutoka Tanzania kwenye hiyo video, kwahiyo mjiandae kwa hilo,” alisema Wizkid alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.
Wizkid ameongozana na Tiwa Savage ambaye mbali na kufanya naye miradi kadhaa ya muziki, wamekuwa washirika wanaoaminika kuwa ni wapenzi wasiotaka kukiri kwa kinywa chao mbele ya umma ingawa wanaonesha mara kadhaa kwa vitendo.
Kenny ndiye aliyepika video ya wimbo mpya wa Diamond ‘Baba Lao’, ambayo ubora wake umeakisi ubora wa kimataifa na huenda ndio sababu Wizkid ameamua kuwekeza pia kupitia mkono wake.
Wizkid ni miongoni mwa wasanii wachache wa Afrika walioweza kushika masikio ya mkondo A wa muziki nchini Marekani na sehemu nyingine duniani. Endapo atakamilisha video yake nchini itakuwa sehemu nzuri ya nyongeza katika juhudi za kuitangaza ardhi ya Tanzania.