YANGA inarejea mzigoni kwenye Ligi Kuu Bara leo Ijumaa kwa kuikabili timu yenye fiziki nzuri ya JKT Tanzania inayonolewa na Kocha Abdallah Mohamed ‘Bares’.
Huo utakuwa mtihani mwingine kwa kocha wa muda wa Yanga, Charles Mkwasa ambae kuna uwezekano mkubwa akapewa nafasi hiyo mpaka msimu umalizike licha ya kwamba makocha kadhaa wanatajwa.
Bares amemwambia Mkwasa kwamba kikosi chake kipo tayari kwa mchezo wa kesho ndani ya Uwanja wa Uhuru na wanaiheshimu sana Yanga kwa vile wanaelewa presha waliyonayo.
“Hakuna ambaye haoni kwa sasa namna ushindani ulivyo, nimewapa majukumu wachezaji na wanayambua kwamba tunahitaji pointi tatu ili kuzidi kujiweka kwenye nafasi nzuri ya ushindani.
“Tunatambua aina ya timu tunayokutana nayo ni ngumu na ina wachezaji wenye uzoefu, hilo halitupi taabu kwani mpira ni dakika 90, tutapambana, mashabiki watupe sapoti,” alisema Bares.
JKT Tanzania ipo nafasi ya sita ikiwa imecheza mechi 10 na pointi zake 15, itamenyana na Yanga iliyo nafasi ya 15, imecheza mechi tano na ina pointi zake 10.