Afya Sio Siasa, Wapuuzeni, Jiungeni Na Vifurushi Vya Bima Ya Afya


Na Mwandishi Wetu-MBEYA
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Albert Chalamila amewataka watanzania kujikatia Bima ya Afya kwa mpango wa vifurushi kuwapuuza baadhi ya watu wanaohusisha siasa na mpango huu ulioletwa kuwafikia watanzania wengi zaidi.

Mhe. Chalamila ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa kampeni za kuhamasisha wananchi kujiunga na vifurushi vya Bima ya Afya katika uwanja wa stendi ya Kabwe, Jijini Mbeya.

Mhe. Chalamila amesema kuwa nchi yoyote ili iweze kujipatia maendeleo katika sekta zote ni muhimu kwa wananchi kuwa na afya bora na ndio maana Serikali imeendelea kuwekeza katika sekta hii ikiwemo kuja na vifurushi vya Bima ya Afya ili kuwafikia watanzania wengi zaidi.

“Ndugu zangu Afya haina siasa, Afya ni uhai tusidanganywe, tujitenge na siasa za kupotoshwa juu ya mfumo huu wa bima, awali kwa mtu mmoja ilikuwa ni lazima uwe na zaidi ya milioni moja ili kuwa na bima ya afya, lakini kwa utaratibu huu wa vifurushi sasa unapata kadi ya bima ya afya kwa shilingi laki moja na tisini na mbili tu”- Alisema Mhe. Chalamila.

Aidha Mhe. Chalamila aliongeza kuwa ugonjwa hauna hodi ni vizuri kila mtanzania kufanya maamuzi ya kujikatia bima kwani wapo watu wengi wamekuwa wakipoteza maisha kutokana na gharama kubwa za matibabu, hivyo mfumo huu wa vifurushi ni suluhisho kwa changamoto hiyo.

Awali akiongea katika hafla hiyo Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Mhe. Anne Makinda amesema kuwa tangu kuzinduliwa kwa mfuko huu muitikio wa watanzania umekuwa ni mkubwa.

Mhe. Makinda amesema kuwa Mfuko upo katika utaratibu wa kuanzisha mpango wa DUNDULIZA ambao utawawezesha watanzania kujiwekeaa fedha kidogkidogo  hadi akamilishe kulipia bima yake.

Pia Mhe. Makinda aliwataka watoa huduma kubadilika na kuwahudumia vizuri wananchi  aendapo kupata huduma za afya kwani mfuko hautotoa kibali kwa hospitali yoyote ambayo itanyanyasa wanufaika wa Bima.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Bw. Christopher Mapunda amesema kuwa uanzishwaji wa Vifurushi ni fursa kwa wananchi kujiunga na bima ya afya kuanzia kiwango cha 192,000 na kuwawezesha kupata huduma ya uhakika ya matibabu hasa kutokana na kuongezeka kwa gharama za matibabu siku hadi siku.

Akiongea baada ya kupatiwa kadi ya Bima ya Afya Bw.  Emanuel Mushi amesema kuwa mpango huu ni mzuri kwani afya ni muhimu na mpango huu wa vifurushi ni mzuri kutokana na kupungua kwa gharama kutoka Milioni moja na laki Tano hadi sasa imepungua na kufikia Shilingi laki moja na tisini na mbili kwa mtu mmoja
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad