Akili za Wabongo na Ufreemason wa Mondi
0
December 23, 2019
“DIAMOND ni Freemason. Pesa zote hizi anapata wapi? Kampa mama yake na mpenzi wake magari ya kifahari? Hapana. Huyu jamaa ana koneksheni na Freemason.” Mbongo mmoja utamsikia akisema hivyo.
Baadaye kidogo utamuona tena msanii mwingine akipita utasikia; “Kachoka, hana pesa wala furaha.” Kisha Mbongo mwingine utamsikia; “Wasanii wetu hawa pesa wanapeleka wapi? Shoo wanapata nyingi, matangazo kila siku. Zama hizi ni tofauti na zamani. Katika zama hizi msanii ukiwa mjanja ni lazima utengeneze pesa nyingi maana fursa zipo. Si unamuona Diamond na Ali Kiba? Si unamuona AY na wenzake! Wamefanikiwa kwa sababu wanajua kujiongeza.
Hao ndiyo Wabongo. Kuna wakati unaweza kushindwa kuwaelewa huwa wanataka nini? Leo wanaponda hiki baadaye wanasifia hichohicho.
Leo wanataka filamu za Kibongo zioneshe uhalisia wa mazingira ya Kiafrika. Akina Sultan Tamba wakiwaletea filamu kali za aina hiyo, filamu zilizojaa visa vya mamamkwe na mawifi, baadhi utasikia wakihoji; “Hizi filamu au maigizo? Hivi tutafikia lini wenzetu wa Hollywood?”
Unataka watu waigize kama akina Van Damme na Chuck Norris, teknolojia iko wapi? Unataka watu waigize kama wako Mitaa ya Miami na Los Angeles, wakati akina Irene Uwoya wakivaa viguo vyao vya ajabu mnaanza kupiga kelele za maadili. Tuwaache Wabongo.
Wabongo wanajidai wanataka watu wafanikiwe kupitia vipaji vyao. Ila wakiona watu wanaanza kupiga hatua, utasikia jamaa huyu mchawi bana. Juzi tu kaanza kuimba, leo tayari ana majumba, biashara na magari kadhaa? Mwingine atampinga. Atasema huyu siyo mchawi, jamaa anauza sembe bana.
Kumbe wakati tunajidai kusema kuwa tunataka watu wafanikiwe, tunakuwa hatuamini kuwa wanaweza kufanikiwa kweli. Historia yetu ya kushindwa kila tunapofanya mambo yetu, inatufanya kuamini kwamba kila mtu akifanya pia atashindwa. Katika hilo ndiyo maana tukaamini marehemu Steven Kanumba alikuwa Freemason. Katika hilo ndiyo maana tunazidi kuhoji mafanikio ya Diamond au Mondi na AliKiba.
Amini nakwambia, Wabongo wengi wanapenda watu wawe katika maisha ya nafuu tu siyo mafanikio makubwa. Ndiyo maana katika hilo, baadhi ya watu waliofanikiwa kwa kiwango kikubwa, wanapewa majina yasiyo mema wala staha.
Mtu hajawahi kuonana hata mara moja na Harmonize ila atakwambia dogo yule anaringa kweli. Umejuaje kama anaringa mtu ambaye siyo tu rafiki yako ila pia unaishia kumuona kwenye runinga na magazeti?
Utacheka pale ukimuuliza akwambie kwa nini anaamini Harmonize anaringa. Atakwambia muone anavyoweka mabega wakati akitembea, muone anavyomposti kila muda yule Mzungu wake.
Tuwavumilie Wabongo. Wakati Mbwana Samatta anatoka TP Mazembe, Thomas Ulimwengu akachukua ufalme wake pale.
Wabongo wakaanza, Ulimwengu kutokana na mwili wake na nguvu zake akitoka tu Mazembe, yule ni moja kwa moja anaenda kama siyo Ufaransa na Italia, basi ni Uingereza kabisa.
Ulimwengu akachukua uamuzi mgumu. Mbali na kuwa anakubalika pale TP Mazembe, kando na kuombwa na Moise Katumbi Chapwe, mmiliki wa TP Mazembe abaki huku akiahidiwa dau nono, akatoka kwenda kuangalia changamoto sehemu nyingine.
Tofauti na Samatta safari ya Ulimwengu imeonekana kukumbwa na changamoto ngumu zaidi baada ya kutoka Mazembe. Alifanikiwa kwenda Ulaya japo siyo katika nchi alizotabiriwa na Wabongo wengi, ila sasa karudi kucheza soka Afrika. Yuko pale Algeria katika Club ya JS Soura. Siyo mfamle kama alivyokuwa Mazembe. Wabongo kwa chinichini wakaanza tena kusema.
Kwamba Ulimwengu aliwahi sana kuondoka Mazembe. Eti angesubirisubiri kidogo ndipo baadaye atoke. Maneno hayo yanatamkwa kwa sababu tu Ulimwengu hajafika pale alipofikiria angekuwepo sasa. Hao ndiyo Wabongo. Hata Samatta angekumbwa na mitihani kama ya Ulimwengu, kauli zingekuwa zilezile. Wabongo bwana!
MAKALA: RAMADHAN MASENGA
Tags