Alichojibu Ester Bulaya juu ya ndoa yake


Dar es Salaam. Mbunge wa Bunda mjini (Chadema) Ester Bulaya ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa ndoa yake na muwe wake Gustavu Babile, bado haijavunjika.

Ni baada ya kuhojiwa na upande wa mashtaka kama ndoa yake imevunjika au laa.

Bulaya ambaye ni mshtakiwa wa tisa katika kesi ya uchochezi inayowakabili, viongozi waandamizi Chadema, akiwamo Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, ameieleza mahakama hiyo leo Jumatatu Desemba 23, 2019, wakati kesi hiyo lilipoitwa kwa ajili ya mshtakiwa huyo kuhojiwa na jopo la mawakili sita wa upande wa mashtaka.

Ameanza kuhojiwa na wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon mbele ya Hakimu  Mkazi Mkuu, Thomas Simba kuhusiana na utetezi wake alioutoa mahakamani hapo, wakati akijitetea.

Wakili Simon amemuuliza mshtakiwa huyo iwapo ndoa yake imevunjika au laa.

Bulaya amedai kwamba, ndoa ya kanisani huwa haivunjiki na kwamba ndoa yake haijavunjika.



Amedai kuwa alifunga ndoa na Balile  mwaka 2003.

Amedai kwa sasa anaishi Mbweni wilayani Kinondoni na Halima Mdee ni jirani yake huko Mbweni.

Akihojiwa na wakili wa Serikali Mkuu Faraja Nchimbi kuhusu hati yake ya kusafiria amedai katika hati hiyo hakuna mahali popote palipogongwa mhuri wa uhamiaji, ukionyesha alisafiri nje ya nchi kati ya Februari 16 hadi 28 mwaka 2018.

Amedai alichoieleza mahakama ni kwamba, Februari 16, 2018, aliwahi kuondoka katika mkutano wa kufunga kampeni kwa kuwa Mdee alikuwa anaumwa hivyo walienda kujiandaa na kwa ajili ya safari ya kwenda kwenye matibabu nchini Afrika Kusini.

Mkutano huo  ulifanyika katika viwanja vya Buibui, Mwananyamala Dar es Salaam.



Alipoulizwa kama kuna sheria yoyote inayoruhusu chama cha siasa kuhamasisha wafuasi wake kudai haki kwa njia ya maandamano au vurugu, amedai hakuna sheria.

"Hakuna sheria inayoruhusu chama cha siasa kuhamasisha wafuasi wake kudai haki kwa maandamano ama vurugu," amedai Bulaya.

Tayari viongozi hao wameshamaliza kutoa utetezi wao kuhusiana na mashtaka yanayowakabili.

Hakimu Simba baada ya kusikiliza utetezi huo, ameahirisha hadi kesi hadi Januari 20, 2020 itakaposikilizwa kwa siku nne mfululizo hadi Januari 24, 2020, ambapo meya wa Manispaa ya Ubungo (Chadema) Boniface Jacob, anatarajia kutoa ushahidi wake siku hiyo.

Mbali na  Mbowe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya jinai 112/2018 ni wabunge wa chama hicho, Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini), John Heche (Tarime Vijijini), Halima Mdee (Kawe) na Esther Matiko (Tarime Mjini).

Wengine ni Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika, naibu katibu mkuu-Zanzibar, Salum Mwalimu na aliyekuwa katibu mkuu wa chama hicho, Dk Vicent Mashinji.

Washitakiwa wanakabiliwa na mashitaka 13 likiwemo la kula njama, ambapo wote wanadaiwa kutenda kosa hilo, Februari mosi na16, 2018, Jijini Dar es Salaam.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad