CCM na Upendo wa Agape Chadema



Huwezi kuamini. Ni vigumu kuwakuta wafuasi wa CCM wakijadiliana na kushauriana na wafuasi wa Chadema juu ya nini cha kufanya ili chama hicho kikuu cha upinzani kisife.

Upendo huu wa Agape huletwa na upepo wa kisulisuli. Mara nyingi nyakati za chaguzi za ndani ya Chadema.

Hii leo eti wafuasi wa CCM wanawashauri wafuasi wa Chadema, kwamba akili na mawazo ya Freeman Mbowe kwa sasa hayawezi kukivusha chama chao na kusonga mbele. Wanataka Chadema watafute mbadala wa Mbowe kwenye uenyekiti, kwa madai kuwa yeye ameishiwa mbinu na sera na hajui nini cha kufanya.

Namna wanavyoelezea faida ya Chadema bila Mbowe, mtu unajiuliza bila yeye wale watu wasingeunga juhudi?

Na upendo huu wa Agape ni mkubwa kiasi cha kutaka kuwapa dola? Chama chenye wabunge zaidi ya 70 unashauri kipate kiongozi mwenye akili mpya ili kifanye nini zaidi? Kichukue nchi? Huu ni zaidi ya upendo?

Bila shaka Lipumba, Cheyo na Lyatonga kuna sehemu hupewa ‘akili mpya’. Ndiyo maana hakuna haja ya vyama vyao kupata viongozi wenye akili mpya.


Pia, tuamini kuwa kuongeza idadi ya wabunge kila msimu ni chanzo cha uchakavu wa akili na sera. Na CDM ni sikio la kufa hawasikii mnadi swala wala muadhini. Wanaichukulia fomu akili chakavu.

Mzee Sumaye kapigwa chini baada ya kuchukua fomu ya kuwania nafasi ya ‘akili chakavu’. Huko Kanda ya Pwani kwa heshima, aliachwa peke yake kugombea uenyekiti. Akaitaka na nafasi maalumu kwa mwenye ‘akili chakavu’ tu kwa kipindi hiki. Kilichompata, ajabu wafuasi wa CCM ndio waliomhurumia zaidi.

Mbali ya kumuhurumia Mzee Sumaye kwa kutoswa ‘kikatili’, Pia wafuasi wa CCM hasa wanakihurumia zaidi Chadema. Kwamba kumtosa Sumaye ni ishara ya kifo chake. Ni upendo wa pekee sana. Ni kama leo hii Simba kuwahurumia Yanga kwa kukosea kuchagua uongozi sahihi kwa klabu.

Chadema ni sikio la kufa. Maana waliambiwa hayahaya wakati wa Chacha Wangwe. Kisha wakashauriwa zaidi kipindi cha Zitto, kwamba kumuondoa kutakigawa chama kama keki ya ‘besidei’. Kubwa kuliko ikawa kwa Dk Slaa alipokisusa chama katikati ya vita. Wakaambiwa chama kitakufa. Bado hakijafa.

Upendo huu wa CCM ulindwe. Ni urithi wa dunia kwa maisha ya demokrasia ya vyama vingi. Wapo wasioelewa faida ya upendo wa Agape. Ni kwamba bila upinzani imara hakuna CCM imara. Lazima wapinzani wapate viongozi imara. Ndio maana ‘akili chakavu’ haitakiwi. Akili mpya huenda akiwa chanzo cha mikutano ya siasa nchi nzima na maandamano.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad