CCM Yawataka Vijana Kuacha Kufoji Umri



Vijana ambao ni wanachama wa Chama Cha Mapinduzi( CCM) wilayani Masasi Mkoani Mtwara wameshauriwa kuachana na tabia hasi ya kufoji umri pindi wanapogombea nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya Chama hicho hasa katika jumuia za umoja wa vijana(UVCCM)

Ushauri huo ulitolewa wilayani humo na katibu wa Itikadi na uwenezi wa Chama Cha Mapinduzi wilaya ya Masasi,Twahili Saidi alipokuwa akizungumza na wandishi wa habari kuhusu lini uchaguzi wa nafasi ya mwenyekiti wa umoja wa vijana wilayani Masasi utafanyika baada ya mwenyekiti wa awali katika nafasi hiyo kutenguliwa kutokana na kubainika kufoji umri wake hivi karibuni.

Alisema CCM wilaya ya Masasi imepokea kwa masikitiko taarifa ya kuondolewa kwa mwenyekiti wa umoja wa vijana wilaya ya Masasi, Azizi Mrope baada ya baraza la vijana la umoja wa taifa kutangaza kuwa mwenyekiti huyo kupoteza sifa yake kutokana na kubainika kuwa wakati akiomba nafasi hiyo mwaka 2017 alifoji umri.

Saidi alisema mapema mwezi huu Disemba 3 baraza la vijana taifa lilitangaza kumuengua mwenyekiti huyo na kuitaka CCM wilaya ya Masasi kutangaza upya uchaguzi wa mwenyekiti umoja wa vijana ili kujaza nafasi hiyo.

Alisema kutokana na jambo hilo CCM wilaya ya Masasi inawataka vijana wote ambao ni wanachama wa Chama hicho kuhakikisha wanapoomba nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya Chama hicho kuacha kudanganya umri wao.

Alisema ni vema wanapojaza fomu mbalimbali za uongozi  kwa ajili ya kuomba nafasi hizo wakajaza umri wao ambao ni sahihi badala ya kudanganya kwa lengo la kutaka kuchaguliwa.

"Kwanza tunaipongeza umoja wa vijana taifa kwa kukaa na kupitia baadhi ya kanuni na kuziboresha lakini pia tunapongeza kwa kuchungza na kubaini mwenyekiti huyu wa umoja wa vijana  wilaya ya Masasi alikuwa amefoji umri wake," alisema Saidi

 Alisema CCM wilaya katika uchaguzi zijazo ikiwemo hiyo ya nafasi ya uenyekiti umoja wa vijana itahakikisha inasimamia kikamilifu suala la umri kwa wagombea wa nafasi hiyo.

 Aidha, katibu huyo wa Itikadi na uwenezi wa CCM wilaya ya Masasi amewataka vijana wa Chama hicho wilayani humo kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi hiyo pindi pale itakapotangazwa rasmi kwa uchaguzi.

Saidi alisema kitendo cha mwenyekiti huyo wa umoja wa vijana CCM wilaya ya Masasi kufoji umri na kupelekea hadi kubainika na kuenguliwa kumeleta funzo kwa vijana wengine wa Chama hicho.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad