Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetetea uamuzi wake wa kushiriki maadhimisho ya miaka 58 ya uhuru wa Tanzania yatakayofanyika kitaifa jijini Mwanza kesho Desemba 9, baada ya kususia kwa miaka mitatu mfululizo tangu mwaka 2016.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Desemba 8, 2019 Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Mambo ya Nje, Itikadi na Uhusiano wa Umma wa chama hicho, John Mrema amesema wametafakari na kuamua kushiriki kwa kuwa wanajiandaa kushika Dola.
“Ni kweli tangu Serikali ya awamu ya tano iingie madarakani hatujawahi kushiriki sherehe za Uhuru. Tumezingatia mambo mbalimbali miongoni ni kwamba sisi ni chama kinachojiandaa kushika Dola na kwa sababu za nyakati na muda ambao tupo, tumeamua kushiriki,” amesema Mrema.
Amesema ujumbe utakaokwenda kwenye maadhimisho hayo utaongozwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.
“Kwa miaka mitatu tumekuwa tukishauriana ndani ya chama, nje ya chama na wadau mbalimbali. Kama chama tumefanya uamuzi wetu tunaamini ni sahihi na baadaye tutawaeleza wanachama wetu kwa kina na mapana,” amesema.
Ameendelea kusema sherehe hizo siyo za CCM bali ni za Taifa, japo kumekuwa na malalamiko ya uminywaji wa demokrasia, lakini wameamua kushiriki hivyohivyo.
“Uhuru wa vyombo vya habari umeminywa, uhuru wa kufanya siasa umeminywa, lakini Wazungu wana msemo unaosema, wakati mambo yanakuwa nmagumu au mazito, watu wazito wanasonga mbele.”
“Tunajua wapo watakaojaribu kupinga, lakini kwa busara yetu, watu wajipange. Katikati ya matatizo makubwa ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa, katikati ya madhila walau tuwe na jambo la kushiriki pamoja la kuunganisha taifa letu kama Watanzania,” amesema Mrema.