Hawa Ndiyo Wenyeviti wa Kanda wa Chadema
0
December 02, 2019
Dar es Salaam. Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania cha Chadema kimepata wenyeviti wa tisa wa kanda huku Kanda ya Pwani ikikosa kiongozi baada ya aliyekuwa mwenyekiti wake, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye kuangushwa katika kura alizopigiwa.
Katika uchaguzi huo uliofanyika Novemba 28, 2019 mjini Kibaha Mkoa wa Pwani, Sumaye aliyekuwa akigombea peke yake alipigiwa kura 28 za ndio na 48 za hapana na kura moja imeharibika. Matokeo hayo yameiacha kanda hiyo ikijipanga kutafuta mwenyekiti mwingine.
Katika kinyang’anyiro hicho kilichokuwa na ushindani mkali, Chadema imepata viongozi wapya wa Kanda wakiwabwaga aliokuwepo.
Miongoni mwa wenyekiti wapya ni pamoja na Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko aliyechaguliwa kuwa mwenyekiti wa Kanda ya Serengeti baada ya kupata kura 44 akimshinda mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche aliyepata kura 38.
Heche ndio alikuwa mwenyekiti wa Kanda hiyo tangu mwaka 2014.
Mbali na Serengeti, Kanda ya Kati nayo imepata Mwenyekiti mpya ambaye ni aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini (CCM) nchini Tanzania, Lazaro Nyalandu.
Nyalandu ameibuka kidedea kwa kupata kura 60 (sawa na asilimia 66.8) kati ya 86 zilizopigwa katika uchaguzi huo akimbwaga aliyekuwa mwenyekiti wa Kanda hiyo, Alphonce Mbasa amepata kura 26 (sawa na asilimia 33.2) uchaguzi huo.
Mwenyekiti mwingine mpya ni Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema wa Kanda ya Kaskazini aliyeibuka kidedea kwa kupata kura 78 akimshinda Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini aliyepata kura 27.
Kanda ya Kusini nayo imepata mwenyekiti mpya ambaye ni Suleiman Methew Luwongo aliyepata kura 53 akimshinda mpinzani wake wa karibu Mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe aliyepata kura 31.
Wengine waliogombea nafasi hiyo ni pamoja na Mansa Nyuchi (kura 3) na Willy Mkapa (kura 02)
Kwa upande wa wenyeviti waliotetea nafasi zao ni pamoja na mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa aliyepata kura 66 akiwashinda wagombea wenzake Sadrick Malila (kura 14) na Boniface Mwabukusi (kura 26).
Pamoja naye, nafasi ya makamu mwenyekiti imechukuliwa na Joseph Sichembe aliyepata kura 57 akiwashinda Sophia Mwakagenda (Mbunge) na Fadhili Shombe.
Mwingine aliyetetea nafasi yake ni mwenyekiti wa Kanda ya Victoria, Ezekia Wenje aliyepata kura 50 akiwashinda wapinzani wake Chifu Kalumuna aliyepata kura 25 na Tungaraza Njugu aliyepata kura mbili.
Wengine waliotetea nafasi zao ni pamoja na Hafidhi Saleh wa Kanda wa Pemba na Said Mzee Said Kanda ya Ugunja.
Pamoja na majukumu kwenye kanda zao, katiba ya Chadema inaeleza wenyeviti wa kanda hizo ni wajumbe wa kamati kuu ya chama hicho
Tags