Kocha Mpya wa Simba Aikataa Ripoti ya Patrick Aussems



IMEFAHAMIKA kuwa Kocha Mkuu mpya wa Simba, Mbelgiji, Sven Vanderbroeck ameuzuia uongozi wa timu hiyo kufanya usajili katika dirisha dogo, akiamini hao waliopo wanatosha kuipa ubingwa wa Ligi Kuu Bara.

 

Hiyo ikiwa ni siku chache baada ya uongozi wa timu hiyo kukutana na kocha huyo kwa ajili ya kujadiliana usajili huo wa dirisha dogo uliofunguliwa wiki iliyopita kabla ya kufungwa Januari 16, mwakani.

 

Wakati kocha huyo akikataa usajili, aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mbelgiji, Patrick Aussems, alipendekeza usajili wa straika mmoja wa kimataifa mwenye uwezo mkubwa zaidi ya Mnyarwanda, Meddie Kagere na nahodha John Bocco.

 

Hata hivyo, licha ya kugomea usajili wa Januari, Championi linafahamu kuwa Simba hivi sasa ipo katika mchakato wa kuongeza straika mwingine.

 

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatatu, kocha hana mpango wa kusajili straika yeyote katika usajili huo wa dirisha dogo akiamini hao waliopo wanatosha kuipa ubingwa Simba na hasa kwa kuwa haina michuano ya kimataifa msimu huu.

 

Mtoa taarifa huyo alisema kama Simba watasajili straika basi siyo mapendekezo ya kocha, watakuwa viongozi ambao bado wana hofu ya safu hiyo kutokana na Bocco kusumbuliwa na majeraha kila wakati huku wakimtegemea Kagere pekee.

 

“Kocha hana mpango wa kusajili mchezaji mpya katika usajili huu wa dirisha dogo baada ya kupendekeza kutosajili mchezaji baada ya kuridhishwa na hao waliopo.

 

“Kama Simba watasajili mchezaji basi yatakuwa mapendekezo ya uongozi baada ya mabosi hao kuingia hofu ya safu ya ushambuliaji ambayo wana hofu nayo inahitaji kuboreshwa,” alisema mtoa taarifa huyo.

Alipotafutwa kocha msaidizi wa timu hiyo, Selemani Matola kuzungumzia hilo, alisema: “Suala la usajili lipo kwa kocha mkuu na viongozi na siyo mimi.”

 

WILBERT MOLANDI, Dar es Salaam



Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad