Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, ameiomba Serikali ya Japan kupitia Shirika lake la Maendeleo ya Kimataifa la Japan (JICA) kusaidia upatikanaji wa fedha kwa njia ya mikopo nafuu kwa ajili ya kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali ikiwemo reli ya kisasa, nishati na kilimo.
Dkt. Mpango ametoa maombi hayo Jijini Dodoma, wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa JICA, Dkt. Nobuko Kayashima, ambapo wawili hao wamejadili masuala mbalimbali yanayohusu utekelezaji wa miradi inayokusudiwa kufadhiliwa na Serikali ya Japan kupitia Shirika hilo.
Amesema kuwa hivi sasa Serikali imeelekeza nguvu na fedha zake za ndani kujenga Reli kwa kiwango cha Kimataifa (SGR), Ujenzi wa Bwawa la kuzalisha umeme kwa njia ya maporomoko ya maji ya Mto Rufiji mkoani Pwani (Nyerere Hydral Power Plant), na kwamba miradi inahitaji fedha nyingi ambazo anaamini Japan inaweza kusaidia upatikanaji wake.
“Tumeanza kutekeleza miradi hii kwa kutumia fedha zetu za ndani na tunaiomba Serikali ya Japan kuzishawishi taasisi zake za fedha kwa kushirikiana na taasisi nyingine kutupatia mikopo yenye masharti nafuu ili tuweze kukamilisha miradi hiyo muhimu kwa Taifa” alisema Dkt. Mpango
Alifafanua kuwa kukamilika kwa miradi hiyo kutaongeza shughuli za kiuchumi na kibiashara hapa nchini pamoja na nchi jirani ambazo hazijapakana na Bahari huku nishati ya umeme ikitarajiwa kuboresha upatikanaji wa umeme kwa ajili ya kuendesha reli hiyo pamoja viwanda