Kiba Akosa Top 10 Bongo Chat...Nini Tatizo



DAR: USHINDANI kwenye sekta ya muziki Bongo Fleva unazidi kuwa mkubwa, mastaa wanachuana kwelikweli kuhakikisha wanashika namba moja, IJUMAA linakuletea ripoti ya mwaka 2019.

 

TOP 10 YA BOOMPLAY

Habari ikufikie kwamba, mtandao maarufu duniani kwa kusambaza kazi za wasanii hasa muziki, Boomplay umetangaza Top Ten (10) yake ambayo staa wa Bongo Fleva, Ali Saleh Kiba ‘King Kiba’ ameibua mshangao mkubwa kwa kuikosa.

 

Boomplay imekuwa ikitoa tathmini za mara kwa mara na kuonesha viwango mbalimbali vya wanamuziki ambapo kwa tathmini waliyoitoa hivi karibuni, Kiba hajaingia kwenye kumi bora ya wanamuziki wanaosikilizwa zaidi (most streamed artist- Tanzania).



ORODHA KAMILI

Mtandao huo katika Kipengele cha Tanzania umeainisha kuwa, namba moja inashikiliwa na staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ au ‘Mondi’.

Namba mbili amepewa Faustina Charles Mfinanga ‘Nandy’. Tatu imekwenda kwa Rajabu Abdul ‘Harmonize’ au ‘Harmo’.

 

Namba nne amepewa Raymond Mwakyusa ‘Rayvanny’. Tano imeshikiliwa na Aslay Isihaka.

Mtandao huo umeainisha, namba Sita inashikiliwa na Mbwana Yusuf Kilungi ‘Mbosso’ huku saba ikienda kwa Juma Mussa ‘Jux’. Namba nane ameishikilia Abdul Idd ‘Lava Lava, namba tisa imekuwa mali ya mwanamuziki wa Injili Bongo, Joel Luaga na aliyefunga top ten ni Vanessa Mdee ‘V-Money’.

 

KIBA AKOSA

Mtandao huo umeishia hapo kwa kuonesha nyimbo hizo kumi bora ambapo Kiba ameshindwa kupenya kutokana na kushindwa kuwapata mashabiki wengi zaidi ya kusikiliza kazi zake.



MTAALAM AFUNGUKA

Akizungumza na Gazeti la IJUMAA, mtaalam wa mambo ya IT, Edwin Lindege amesema wanachokifanya Boomplay katika kupima nyimbo ni idadi ya watu wanaosikiliza nyimbo za mwanamuziki husika ambazo kwa pamoja zinamfanya mwanamuziki fulani aweze kuongoza na mwingine ashindwe.

 

“Wale wenyewe wanapandisha nyimbo za wasanii, hivyo wana uwezo wa kujua wimbo umesikilizwa mara ngapi hivyo inakuwa rahisi kwao kujua nyimbo kadhaa za mwanamuziki fulani zimesikilizwa na watu wangapi kwa ujumla wake na ndio maana unaona wanatoa orodha ya wanamuziki wanaoongoza kwa kusilizwa kwa kipindi husika,” alisema Lindege.

 

HAKUNA LONGOLONGO?

Lindege aliongeza kuwa, kwenye ‘dunia ya mitandao’, data au namba zinaongea na hakuna longolongo kwani kipimo cha mtu kuwazidi wenzake kinatokana na majibu kutoka kwa watazamaji au wasikilizaji katika mtandao husika.

 

“Hakuna longolongo, ni kama vile unavyoona video imetazamwa na watu wangapi katika Mitandao ya YouTube, Instagram au Facebook.

“Views (watazamaji) wanaonekana pale na kila mtu anaona. Sasa wao wanajumlisha na kupata matokeo ya moja kwa moja,” alisema mtaalam huyo.

 

AFRIMMA WAMBEBA ZAIDI MONDI

Katika hatua nyingine, orodha nyingine mpya iliyotolewa na jarida maarufu Afrika (African Muzik Magazine -AFRIMMA) la nchini Nigeria limeainisha Top Ten ya Wanamuziki Bora Afrika kwa mwaka 2019 kupitia ukurasa wao wa Instagram ambapo Mondi wamempa nafasi ya nne.



WAPOSTI MOJAMOJA

Kwenye ukurasa huo, wameanza kwa kuposti namba kumi ambayo imeshikiliwa na Aya Nakamura, tisa imeshikiliwa na Busiswa Gqulu na nane ikaenda kwa Sho Madjoz huku saba ikishikiliwa na Yemi Alade.

 

Namba sita wamempa Tiwa Savage na Tano ni Fally Ipupa.

Orodha hiyo imeendelea ambapo namba nne ni Diamond, namba tatu amepewa Wizkid na namba mbili ni Davido.

 

Namba Moja waliwaacha wafuatiliaji wao waendelee kubashiri ni nani, lakini hata hivyo, IJUMAA linafahamu kuwa kwa asilimia kubwa nafasi hiyo itakwenda kwa mkali wa Nigeria, Damini Ebunoluwa Ogulu maarufu kama Burna Boy.

Stori: Waandishi Wetu, Dar

 



Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad