Kilio Cha Wananchi Kuhusu Bima ya Afya Chasikika...Waziri Afunguka Haya....



Aveline Kitomary -Dar es salaam

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema wizara hiyo kwa kushirikiana na Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) inaendelea kuboresha vifurushi vya bima ya afya kwa kuweka magonjwa yenye gharama kubwa kama moyo, figo, saratani, kisukari na mengineyo.

Akizungumza jana Dar es Salaam, Ummy pia alisema katika vifurushi hivyo huduma ya uzazi itaendelea kuboreshwa kwa kupunguzwa muda wa kusubiri matumizi.

Katika vifurushi vya sasa, mbali na gharama kubwa ya bima, pia baadhi ya wananchi wanalalamikia kitendo cha magonjwa ya moyo, baadhi ya vipimo vya moyo na figo kutokuwapo kwenye vifurushi hivyo.

Akizungumzia hali hiyo jana, Ummy alisema; “haya ni maeneo ambayo tunaboresha, mwanzo walikuwa hawajaweka nikawaambia inabidi yawepo, maana ya bima ukipata tatizo la figo upate matibabu, sisi tumewaachia Bodi ya NHIF wafanyie kazi, lakini na sisi wizara tunaendelea kupokea maoni na ushauri na kuwaambia warekebishe.

“Lakini kuhusu magonjwa yasiyo ya kuambukiza tunatakiwa kuwekeza katika kinga, hivi karibuni Waziri Mkuu alizindua kampeni ya mpango wa taifa wa kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyo ya kuambukiza, tutaendelea kutoa elimu ya kujikinga.

“Tutaanza kampeni hata kwenye lifti, tutaandika tumia ngazi badala ya lifti, tutatafuta ‘parking’ (maegesho ya magari) za mbali ili watu wenye magari watembee, tunahimiza kufanya mazoezi, aina za ulaji na tutahimiza watu kuepuka matumizi ya pombe na sigara.

“Lakini hili la wajawazito nakubaliana na wewe, hata mimi niliona, lakini lengo lake sio kwamba leo nina ujauzito wa miezi saba unaenda kukata bima, lengo lake ni watu wakate bima kabla ya kupata ujauzito, lakini miaka hiyo itapunguzwa, nikawaambia NHIF isiwe miwili, tusipoweka masharti kuna watu wanaenda kukata bima wakiwa wajawazito, lakini bado miaka miwili ni mingi.

“Sisi kama wizara tunaendelea kutoa maelekezo kwa NHIF kuendelea kupokea maoni na kuboresha vifurushi. Mfano hii ya wajawazito nikawaambia kuwa miaka miwili ni mingi, kwahiyo wapunguze, lakini haitaki mtu akiwa mjamzito apate bima, nikawaambia rudisheni angalau iwe mwaka mmoja kushuka chini.”

Ummy pia alisema baada ya kupitisha sheria ya bima ya afya kutokana na watu wengi kutumia, gharama za bima hizo zitapungua hivyo maboresho yanaenda hadi kwenye gharama.

“Lakini mbeleni mwelekeo wetu kuhusu bima ya afya tunaendelea kufanya mchakato kutunga sheria ambapo bima ya afya itakuwa lazima na baada ya hapo gharama zitapunguzwa kwa sababu watu wengi watajiunga.

“Kilichotukwamisha mpaka sasa ni mawazo ya kuunganishwa na Mfuko wa Fidia ya Wafanyakazi (WCF), hapa kuna sheria za Shirika la Wafanyakazi Duniani (ILO), lakini nataka kabla ya Bunge la mwezi wa pili tutaenda na hiyo sheria bungeni,” alisema Ummy.

Kuhusu gharama kubwa ya vifurushi vya bima kwa wazee, Ummy alieleza bado kuna sera ya kutoa matibabu ya bure kwa wazee ambao hawana uwezo.

“Kuhusu gharama kubwa za wazee, hii inatokana na kuangalia hali halisi ya wazee kuumwa mara kwa mara, lakini kwa wazee wasio na uwezo bado kuna sheria ya afya haijabadilika, wanatakiwa kupata matibabu bila malipo, inaruhusu kupata matibabu bure,” alisema Ummy.

Hata hivyo alisisitiza kuwa huduma za bima ya afya jamii bado hazijabadilishwa, hivyo kuwataka watumiaji wasiwe na wasiwasi.

“Jambo lingine ninalolisisitiza bado huduma ya bima ya jamii ipo, CHF ipo na tumeboresha, zamani ilikuwa inatumika katika halmashauri moja, sasa hivi inatumika halmashauri zaidi ya moja,

tumeelekeza pia ikubaliwe mpaka hospitali ya mkoa,” alisema Ummy.

Pia alisema utaratibu wa msamaha kwa watu ambao hawana uwezo wa kulipia matibabu bado unaendelea na kutaka wahusika kufuata utaratibu.

“Bado hatujaondoa utaratibu wa Serikali kugharamia watu wasio na uwezo. Utaratibu wa msamaha kwa watu bado unaendelea, kuna baadhi ya watu wanataka kufanya siasa, kuhusu hili nataka niwaambie Serikali inatoa fedha nyingi kwa ajili ya msamaha.

“Niendelee kuwatoa hofu Watanzania kuwa utaratibu wa msamaha uko pale pale, pili utaratibu wa bima ya afya ya jamii bado unaendelea na tatu tunatumia sheria ya lazima bima ya afya itawekwa na gharama zitapungua,” alisema Ummy.

Aliwaagiza NHIF kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu vifurushi vipya vya bima ya afya.

“Kwenye vifurushi vya bima ya NHIF kuna upasuaji, kubwa ni kuendelea kutoa elimu kwa wananchi, mfano akiwa na vifurushi anapata aina 14 za upasuaji.

“Nimewaelekeza NHIF kuendelea kutoa elimu, lakini pia maelekezo niliyotoa ni wananchi kulipia kwa awamu angalau mara tatu au nne, baada ya hapo mtu anapata bima yake,” alisema Ummy.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad