Ni ukweli kwamba wako wanawake wengi sana ambao wanahesabu kuwa ni baraka na jambo la kumshukuru Mungu kwa kuwaumba wenye sura nzuri na wenye mvuto. Pamoja na ukweli huu, ni wazi na imethibitika kwamba wako wanawake ambao wanahesabu kuzaliwa warembo ni mojawapo ya laana au mkosi kwasababu ya zile hali ambazo wamezipitia hususani katika mahusiano yao ya kila siku na wanaume.
Mara kwa mara kumekuwepo na tabia ya wanaume kutamani sana kuwa kwenye mahusiano na wanawake warembo, na hupenda kuwatongoza hao mara kwa mara ingawa moyoni mwao wanawaangalia warembo hawa kama wasichana wa kula nao raha tu “good time girls” na wala sio wake wakuoa.
Utakubaliana na mimi labda umewahi kuona mwanaume anakuwa kwenye mahusiano na binti mzuri sana kisura na kiumbo tena wanakuwa kwenye mapenzi kwa muda mrefu tu huku huyu binti akijua mbeleni kuna ndoa, ghafla ukija kusikia huyu kaka anaona unapigwa mshangao kuona wala sio yule binti mrembo anayeolewa.
Hii imewaacha mabinti wa aina hii katika maumivu makali sana ya moyo, na wengine wamekata tama na kuamua kujirahisisha ili mraadi maisha yaende. Wengine wameamua kukaa wakitunzwa na waume za watu kwasababu wao wamejithibitishia kwamba kuolewa hakupo.Tafiti zinaonyesha kwamba ukiona mwanaume aliyeamua kukaa muda mrefu na mwanamke mrembo, mara ningi unakuta ni wale wanaume wenye tabia za kisanii “players” ambao hata wao huwatumia mabinti hawa na kuwatelekeza hapo baadae.
Inasemekana imani au mtazamo huu hauko tu kwa wanaume bali hata wanawake wale wenye uzuri au urembo wa kati au wasio warembo kabisa wanajua na kuamini hivyo na mara nyingine huwarushia vijembe wale wanawake warembo kuwa “utachezewa tu na utaachwa na wataolewa wengine”. Na pale inapotokea kwenye mahusiano binti wa kawaida akagundua mpenzi wake wa kiume ametembea au husiana kinyemela na binti mrembo zaidi kuliko yeye, utakuta wakikutana kwenye kupashana au hata kwenye ugomvi wa kuandikiana ujumbe wa maneo, huyu binti wa kawaida humwambia yule mrembo kwamba “we jifurahishe tu ila usiamini kwamba utaolewa, huyu mwenzako anakuchezea tu anajuwa nani wa kuoa”. Unadhani imani hii wameitoa wapi?
Wakati mfumo au mtazamo huu unapoenea au kujirudia zaidi, wanawake hawa warembo au wazuri wa sura na umbo huamini kwamba wanaume wote ndivyo walivyo, wanaamini kwamba wanaume wote huwasogelea ili kujifurahisha kimapenzi tu na baada ya hapo kuwakimbia. Wakati huu wa kusubiria kumpata mwanaume wa kuoa “Mr. Right” ukizidi wanawake hawa huchoka na kukata tama, na hivyo wao sasa huamua kukimbizana na kutafuta mwanaume wa kuwapenda na kutulizana nao.
Tabia hii ya kuwafukuzia wanaume kwa bahati mbaya kuwagharimu sana wanawake hawa kwasababu wanaume wengi wanamtazamo hasi kwa wanawake wa jinsi hii. Wanaume wengi wanaamini wao ndio wanatakiwa kuwa wa kwanza kumtongoza mwanamke na sio mwanamke kuwa wa kwanza kuwatongoza wao, na mbaya zaidi anapokuwa mwanamke mzuri ndio shida huongezeka, wengine wakianza kuambiana “huyu lazima atakuwa mgonjwa anataka kuambukiza wengine”. Hapa unaweza kuelewa ni kwa kiasi gani hali huwa ya kutatiza.
Kwa upande mwingine, wanawake hawa wanaoonekana wazuri wa umbo na sura, sio halisi kama wanavyoonekana. Kwa mbali ni kweli mwanaume yeyote atavutiwa nao lakini jinsi unavyowakaribia na kuwafahamu unagundua mengi yanayohuzunisha na kuogopesha kuishi nao. Unagundua kuwa uzuri mwingine umeongezewa kutoka madukani zaidi na sio ulio halisi. Mara nyingine uzuri huu na ile hali ya kuonekana ni wagharama sana huwaogopesha wanaume wasio na kipato kikubwa na kwahiyo wanaume hawa wakishapata kabahati ka kufaidi penzi mara moja au mbili wanakimbia tena kwa kasi wakihofia kukamuliwa kiuchumi, ingawa mara nyingine hofu yao hii huwa sio ya kweli. Inasemekana baadhi ya wanawake wa aina hii huwekeza zaidi kwenye kuonekana wazuri na walimbwende ili kuficha au kufunika baadhi ya mapungufu yao.
Wanaume wengi walioulizwa sababu za kuwatumia na kuwatelekeza wanawake wa jinsi hii walisema kuwa, kwa kutembea, kuonekana nao au kufanya nao mapenzi, wanaume hawa hujihisi sifa sana, hususani wanapoonekana na wanaume wenzao, yani ni kama vile timu ndogo iliyopata nafasi kucheza katika kombe la dunia. Unajua tena wanaume wanavyopenda kujionyesha wanapokuwa na wanawake wazuri mbele ya macho ya wanaume wenzao.
Wamesema kwamba wanapowaza kuishi na wanawake hawa kama mume na mke, huwa wanazidiwa na hofu ya kuelemewa au kujihisi kutokuwa salama “sense of insecurity”. Mioyoni mwao wanahisi kwamba kama wanaume wenye hela wamekuwa wanamfuatilia kwa kasi kubwa hivi mwanamke huyu, vipi nikishaoana naye?? Si ndiyo kila siku kusuguana na kukorofishana vishawishi vinapozidi? Je nitaweza kustahimili?
Wanaume wengine walioulizwa walijibu kwamba, wanawake wa jinsi hii ni wa gharama sana, sio rahisi kuwaweka mjini na kuhakikisha wanaishi maisha yao ya kawaida kama hauna fedha ya kutosha. Hata wale wanaume wachache waliokuwa na hao wanawake kwa muda wa maswali haya wameeleza jinsi wanavyohisi wanatumia fedha nyingi na yamkini zaidi ya wanavyojiweza.
Wanawake wa aina hii watahitaji mitoko ya nje ya mji, sehemu zilizojitenga, sehemu za faragha ambazo ni za bei ghali, wanataka zawadi za gharama, ukitaka kuwapa zawadi za kushtukiza “surprise” basi ujipange, sio vitu vya kitoto vitakavyomsisimua aweze kukwambia “waoooooow…this is wonderful” hapo lazima ujipinde mfukoni haswa.
Ukitaka kuwatoa nje kwa ajili ya chakula cha jioni basi lazima kwenda maeneo wanayoenda watu maarufu, mkitaka kwenda kupumzika kidogo nje ya nyumbani basi uwaambie wachague wao wapi pa kwenda, na hapo utakapotajiwa ni pa gharama kubwa sana, na imeelezwa kwamba pamoja na mambo yote haya ya gharama kubwa bado huko wapenzi hawa wanapoenda msichana huyu anaishia kuonekana ni mwanafunzi asiyejua tendo la ndoa kabisa tofauti na hali aliyoionyesha “poor perfomer”, wanaume wengine wanasema inaonekana kama kupoteza tu pesa, unaishia kutokufurahia penzi lenyewe.
Na wengine wameenda mbali zaidi kueleza kwamba hata unapotaka kuzaa na mwanamke wa jinsi hii basi yeye anataka mtoto mmoja au wawili tu akiogopa asije kuliharibu umbo lake, tofauti na kiu ya mwanaume ya kupata watoto zaidi ya wawili. Imeelezwa kuwa hata ujuzi wa kupika kwao ni shida maana kutwa kucha wako “bize” na sura zao, na hata ukikaa nao sio watu wakufurahisha zaidi ya kutumia tu hela zako “they are boring”.
Pamoja na uchunguzi huu na ukiangalia hali halisi ya maisha yetu ya kila siku tena katika jamii tofauti utagundua kwamba wanaume kiu yao sio kuoa wanawake wenye umaarufu, au wenye kujulikana sana, au walio warembo kupindukia, bali wanaume wanapotaka kutafuta mke wa kuoa wanaangalia tabia na haiba zilizojificha, wanauliza tabia ya huyo msichana, wanataka kujua anavyohusiana na watu, wataangalia nyendo zake kuanzia wakati anasoma.
Ni ngumu kuwakuta wamenaswa na aina ya wanawake ambao wanataka kuonekana wakati wote, wanataka wajulikane kuwa wao nao wapo kwenye makundi ya watu, la hasha. Kiu zao ni kuwa na mwanamke ambaye atakuwa mke anaye leta furaha nyumbani, anaye sikiliza, anaye weza kushauri na kushaurika, aliyeko tayari kufundishika sio kuwa mwalimu kwenye kila kitu, anayeweza kuandaa mapishi mazuri yatakayo wafurahisha watoto na mume wake, sio kila siku kuelekeza kipikwe nini wakati yeye analinda kucha zake zisiharibike.
Hivi umewahi kujiuliza kwanini watu wengi waliooa wakiwa na michepuko, hiyo michepuko ni mabinti warembo na walimbwende ila hawajaolewa, hivi hujajiuliza kwanini hawajaolewa? Na hata wengine wakiolewa hizo ndoa kila siku tia maji tia maji, wataachika leo na kuolewa kesho na kuachika kesho kutwa nakuolewa tena mtondogoo.
Unadhani hawa wanaume wanaoenda kwa hao wanawake ni kwamba hawajui wanachokitaka? utashangaa hata umpe mapenzi gani bado hawezi kukwambia atakuoa, ingawa yuko tayari akupangishie nyumba au hata akujengee lakini ulale huko mwenyewe, yeye anaenda kulala na mke wake. Ushauri wangu wa bure kwa wanawake wa jinsi hii; badilikeni tabia zenu, jitihada mnazotumia kwenye kucha na sura zenu ziwekeni kwenye kushuhulikia tabia na haiba zenu, la sivyo mtasubiri sana tu.
Dr. Chris Mauki
UDSM & University of Pretoria. SA
chrismauki57@gmail.com
hii ni tabia ya mtu tu
ReplyDeleteHuo ndio ukweli wanawake wengi Wanaojiona ni Wazuri Wa sura na umbo, huwa nigharama ,yaani wanapenda vitu vya kifahari sana,tutawatumia tu then kuoa!! Hilo tutajua nani ataolewa.
ReplyDeleteNi tabia ya mtu ila kwa utafiti wangu naweza sema a good number of them huwa very insecure na quite narcissitic to say the least
ReplyDelete