KAMA ilivyowahi kutokea kwa aliyekuwa bosi wake kwenye Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB), Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, madaktari wamemuonya staa wa Bongo Fleva, Rajab Abdul ‘Harmonize’.
Onyo hilo linakuja siku chache baada ya kuwepo kwa tetesi kuwa Harmonize au Harmo anafanya kazi muda mwingi kiasi cha kukosa muda wa kupumzika na kujikuta akisumbuliwa na uchovu kupita kiasi ambapo hali hii kitaalam huitwa Fatigue.
Hali hii aliwahi kukutana nayo Diamond au Mondi na kushauriwa na madaktari awe na muda mwingi wa kupumzika.
Kwa upande wake Harmo anadaiwa kukutana na hali hiyo baada ya kufanya shoo mfululizo bila kupumzika.
Usiku wa Desemba 8, mwaka huu, Harmo alifanya shoo ya kihistoria jijini Dar kisha alfajiri yake alitimkia jijini Mwanza kwenye Shoo ya Sikukuu ya Uhuru Desemba 9.
Usiku wa Desemba 9, Harmo alifanya tena shoo jijini Mwanza kabla ya kutimkia mkoani Shinyanga ambako nako aliangusha shoo ya nguvu.
Pia ukitazama ratiba ya shoo zake kwa mwezi Desemba zinaonesha baada ya Shinyanga atarejea jijini Dar kufanya shoo kubwa kwenye Viwanja vya Tanganyika Packers.
Baada ya hapo atakwenda kufanya shoo Muleba mkoani Kagera, Tandahimba mkoani Mtwara, Mombasa na Naivasha nchini Kenya.
Kufuatia hali hiyo, baadhi ya madaktari waliozungumza na Gazeti la IJUMAA walimuonya Harmo au Konde Boy.
Kwa mujibu wa madaktari hao, watu wengi hupata Fatigue kutokana na shughuli zao za kila siku bila kujua hali hiyo huwasababishia athari mbalimbali kimwili na kiakili.
Walisema Fatigue ni hali ya uchovu ambayo mtu huhitaji mapumziko kutokana mwili kukosa kuchoka na husababishwa na kufanya kazi kwa muda mrefu bila kupumzika, kutopata muda wa kulala, hofu, kutofanya mazoezi au uchovu.
Kwa mujibu wa Dk Isack Maro ambaye ni Mkurugenzi wa Hospitali ya TMH ya jijini Dar, mtu anayepatwa na hali hiyo yupo kwenye hatari ya kuamsha maradhi aliyokuwa nayo hata kama yalitulia.
Alisema kama mtu ana shinikizo la damu au sukari inaweza kupanda kwa sababu mwili unakuwa dhaifu.
“Ndiyo maana watu wanaoumwa maradhi kama hayo na mengine, hutakiwa kupata muda mwingi wa kupumzika kuepuka mambo kama hayo,” alisema.
Naye Dk Godfrey Chale wa Hospitali ya Temeke jijini Dar, alisema aghalabu Fatigue husababishwa na kufanya kazi kupita kiasi na kuchoka. Alisema wanaofanya kazi zenye hekaheka nyingi na wanaofanya mambo mengi kwa wakati mmoja, hukumbwa na uchovu kupita kiasi.
Akizungumzia hali hiyo inayompata Harmo, Mtaalam wa Saikolojia ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Chris Mauki alisema, hali hiyo hutokana na mwili kufanya kazi kupita uwezo wake au muda mrefu bila kupumzika, hivyo akili kufanya kazi kuliko uwezo wa kawaida na kuumiza hisia pia.
“Kwa kawaida kuna baadhi ya vitu mwilini hufanya kazi pamoja. Kazi karibu zote huhusisha akili na hisia kwa sababu bila akili huwezi kujua unafanya nini na bila hisia huwezi kufanya maamuzi ya unachokifanya kwa wakati huo.
“Hivyo anachotakiwa kufanya ni kwamba kama amechoka kwa kufanya kazi muda mrefu, akili na hisia pia zinachoka kwa sababu vinashirikiana. Hivyo anahitaji mapumziko ya muda mrefu,” alisema Dk Mauki.
Stori: Waandishi Wetu, Dar