Madaktari Wanaoshutumiwa Kuwatolea Mimba Wagonjwa Washitakiwa Kuhujumu Uchumi



Daktari wa magonjwa ya binadamu anayejulikana kwa jina la Awadhi Juma (40), ambaye ni mfanyakazi wa hospitali binafsi ya dental clinic, iliyopo Sinza Mori, Dar es Salaam pamoja na muuguzi mmoja anayefahamika kwa jina la Kidawa Ramadhani (26), leo Desemba 27, 2019 wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashtaka saba likiwamo la kutoa mimba wagonjwa na kutakatisha fedha kiasi cha shilingi 260,000.

Washtakiwa hao wamefikishwa mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mkazi, Vicky Mwaikambo, ambapo kabla hajawasomea mashtaka yao alisema washtakiwa wote wawili hawatakiwi kujibu chochote kwakuwa Mahakama ya Kisutu haina uwezo wa kusikiliza kesi za uhujumu uchumi isipokuwa kwa kibali maalumu kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka Serikalini (DPP).

Akisoma hati ya mashtaka, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon akisaidiana na Glory Mwenda, amedai washtakiwa hao wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 139/2019.

Wakili huyo Mwandamizi wa Serikali ameiambia mahakama kuwa katika tarehe tofauti mwezi Oktoba 2019 eneo la Sinza Mori, Dar es Salaam, washitakiwa hao wakiwa na lengo la kumtoa mimba mgonjwa, waliingiza bomba la sindano katika uke wa mgonjwa F.R na S.S, hali iliyosababisha kuharibika kwa mimba.

Aidha Wakili huyo wa Serikali ameongeza kuwa katika tarehe tofauti, Agosti 2012, jijini Dar es Salaam, mshtakiwa Daktari Juma kwa lengo la kudanganya, alighushi cheti cha stashahada cha utaalam wa tiba ya kinywa akionesha ni halali na kimetolewa na Chuo cha Tiba cha Muhimbili wakati akijua si kweli.

Katika shtaka la kutakatisha fedha, Wakili Wankyo Simon amesema Daktari Juma anadaiwa kati ya Mei 2015 na Desemba 4, 2019 alijipatia shilingi 260,000 wakati akijua fedha hizo ni zao la kosa la jinai la kugushi.

Hata hivyo, Wakili huyo Mwandamizi wa serikali amesema kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika, jambo lililomfanya hakimu Mwaikambo, kuahirisha kesi hiyo hadi Januari 10, 2020, ambapo shauri hilo litatajwa tena.

Washitakiwa wamerudishwa rumande kutokana na shtaka la kutakatisha fedha kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria nchini Tanzania.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad