Marekani Yazindua Rasmi Jeshi lake Jipya la Anga za Juu
0
December 22, 2019
Rais Donald Trump amesaini pesa za kuwezesha mradi mpya wa Pentagon, jambo ambalo linarasimisha kuanzishwa kwa kikosi cha vita vya anga za juu- kifahamikacho kama US Space Force.
Kikosi hicho kipya katika jeshi la Marekani, ni kikosi cha kwanza katika huduma za jeshi la Marekani kwa miaka 70, na kiko chini ya jeshi la anga la Marekani.
Katika ngome ya kijeshi karibu na Washington, Bwana Trump alielezea anga za juu kama "eneo jipya la dunia la mapigano ya kivita".
"Huku kukiwa na ongezeko kubwa la vitisho kwa usalama wa taifa letu , ukuu wa Marekani katika anga ni muhimu sana," alisema.
"Tunaongoza, lakini hatuongozi vya kutosha, lakini muda mfupi sana tutakua tunaongoza kwa kiwango kikubwa."
"Jeshi la anga za juu litatusaidia kuzuwia uchokozi na kudhibiti anga za juu ," aliongeza.
Pesa zilizotengwa kwa ajili ya shughuli za kikosi hicho zilithibitishwa Ijumaa wakati rais Trump aliposain dola bilioni 738 sawa na pauni bilioni 567 za bajeti ya mwaka ya jeshi la Marekani. Uzinduzi huo utagarimu dola milioni 40 kwa mwaka wa kwanza.
Marekani imesema hailengi kuweka majeshi yake katika uzio wa dunia, lakini italinda mali za Marekani - kama vile mamia ya satelaiti zinazotumiwa kwa mawasiliano na uchunguzi.
Hii inakuja wakati wakuu wa jeshi la Marekani wakiyaona mataifa ya Uchina na Urusi yakijiimarisha kijeshi.
Makamu wa rais wa Marekani Mike Pence awali alisema kuwa mataifa hayo mawili yana ndege za kemikali zinazoweza kuangusha makombora mara baada ya kufyatuliwa na makombora yanayoweza kulipua setilaiti ambayo Marekani inahitaji kukabiliana nayo.
"Mazingira ya anga za mbali yamebadilika sana ikilinganishwa na nyakati za vizazi vilivyopita," alisema. " Kile kilichokua mazingira ya amani na yaziyoshindaniwa kwa sasa kimejaa upinzani ."
Kikosi cha anga za juu cha Marekani kitaanza shughuli zake kwa kuzingatia ushauri wa kituo kilichopo kwa sasa cha maagizo ya kijeshi ya anga za juu (SpaceCom) , ambacho kilibuniwa mwezi Agosti kushughulikia operesheni za jeshi la Marekani za anga za mbali.
Mkuu wa kikosi cha anga cha Marekani Barbara Barrett alisema kuwa kikosi cha anga za juu kitajumuisha wanajeshi wa anga 16,000 na wafanyakazi wa kawaida.
Kitaongozwa na Generali wa Kikosi cha anga Jay Raymond, ambaye kwa sasa anaongoza kituo cha anga za juu -SpaceCom.
Mapema mwezi huu rais wa Urusi Vladimir Putin alisema kuwa hatua ya Marekani ya kupanua uwepo wake katika anga za juu ni tisho kwa maslahi ya Urusi, na inahitaji jibu kutoka kwa Urusi.